Chelsea shida ni mishahara

Muktasari:
- Chelsea imekuwa ikimtegemea Nicolas Jackson kama mshambuliaji wao wa kati, lakini mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 msimu huu amefunga mabao tisa tu na kutoa asisti tano katika mechi 26 za michuano yote.
LONDON, ENGLAND: LICHA ya kufanya kazi ya ziada kwa ajili ya kutafuta mshambuliaji mpya kuelekea dirisha lijalo, ripoti zinaeleza wanakumbana na ugumu wa kumsaini mshambuliaji wa kiwango cha juu kutokana na mshahara ambao wapo tayari kuutoa.
Chelsea imekuwa ikimtegemea Nicolas Jackson kama mshambuliaji wao wa kati, lakini mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 msimu huu amefunga mabao tisa tu na kutoa asisti tano katika mechi 26 za michuano yote.
Mbali ya kiwango cha Jackson moja kati ya sababu zinazochangia Chelsea kutaka kusajili mshambuliaji mpya ni kuomba kuondoka kwa Christopher Nkunku mwisho wa msimu huu.
Tovuti ya Sky Sports imetaja majina kama Liam Delap wa Ipswich Town, Hugo Ekitike wa Eintracht Frankfurt, Benjamin Sesko wa RB Leipzig, na Jonathan David wa Lille kuwa miongoni mwa wanaohusishwa na Chelsea.
Lakini wachezaji hao pia wamehusishwa na baadhi ya timu kubwa zaidi barani Ulaya, zikiwemo baadhi za Ligi Kuu England.
Na kwa mujibu wa tovuti ya Daily Mail, Chelsea huenda wasiweze kushinda katika vita hiyo kwa sababu ya suala la mishahara.
Chanzo hicho hicho kinadai kuwa mmoja kati ya wachezaji tajwa hapo juu alikataa uhamisho wa kwenda Stamford Bridge baada ya kutoridhishwa na mshahara walioahidi kumpa ambao ulikuwa mdogo ukilinganisha na hata ule wa baadhi ya timu za madaraja ya kati za England ambazo walimwekea mezani.
Wakala wa mchezaji huyo alisema: "Chelsea hawalipi mishahara."
Chelsea wamekuwa wakitumia fedha nyingi sana tangu Todd Boehly na Clearlake Capital walipochukua usimamizi kutoka kwa Roman Abramovich majira ya joto ya mwaka 2022.
Takwimu kutoka ripoti ya kila mwaka ya European Club Finance and Investment Landscape zilionyesha kuwa Chelsea ilikuwa na kikosi ghali zaidi kuwahi kurekodiwa kwenye upande wa ada za usajili mwaka 2024.
Mwisho wa mwaka wa kifedha, Chelsea walikuwa wametumia kiasi cha Euro 1.7 bilioni kwa jumla ya gharama za usajili.
Hata hivyo, taarifa za ndani zinaeleza wamekuwa wakitoa tu ada kubwa lakini sio mishahara mikubwa.