Chelsea inatafuta uwanja

LONDON, ENGLAND. JIRANI yako ndio nduguyo wanasema. Ndicho unachoweza kusema baada ya Chelsea kuripotiwa kuwa na mpango wa kuwafuata wapinzani wao kwenye Ligi Kuu England, Fulham kwenda kuwaomba watumie uwanja mmoja wa mechi zao za nyumbani wakati watakapofanya maboresho ya Uwanja wa Stamford Bridge.

The Blues wanapanga kuwaomba Fulham ili watumie Uwanja wa Craven Cottage kwa kipindi cha miaka minne kwa mechi zao za nyumbani kwenye Ligi Kuu England.

Mmiliki wa Chelsea, bilionea Todd Boehly na mmiliki mwenza, Behdad Eghbali wamepanga kuifanya The Blues kuwa moja ya timu zenye viwanja matata kabisa duniani hadi ikifikapo mwaka 2030.

Kinachoelezwa ni kwamba Chelsea kwa sasa ina machaguo matatu juu ya mipango ya uwanja wao itakaotumia kwa ajili ya mechi zao za nyumbani.

Chaguo la kwanza la mpango wao ni kujenga uwanja mpya kwenye eneo jipya kabisa. Chaguo la pili la mpango wao ni kuubomoa wote Stamford Bridge na kuujenga upya kabisa, wakati mpango wao wa tatu ni kuufanyia tu maboresho Stamford Bridge na kuufanya kuwa kwenye mwonekano wa kisasa.

Iliwahi kuripotiwa kwamba klabu hiyo ya London Magharibi ilipanga kuuvunja uwanja wote wa Stamford Bridge na kisha kuujenga upya kwenye eneo hilohilo na hicho ndicho kinachodaiwa kwamba kitafanyika.

Mradi mzima wa ujenzi wa Stamford Bridge mpya utagharimu Pauni 2 bilioni na kwamba katika kipindi cha ujenzi wake, ambao unatazamiwa kuwa wa miaka minne, Chelsea italazimika kutafuta sehemu ya kwenda kucheza mechi zao za nyumbani.

Na hapo kinachoelezwa ni kwamba Chelsea huenda ikaenda kutumia uwanja wa nyumbani wa Fulham, Craven Cottage ama wa Twickenham au Wembley.

Na sasa, inaelezwa Boehly amemfuata Mmarekani mwenzake, bilionea Shahid Khan, ambaye ni mmiliki wa Fulham kuwasilisha maombi ya timu yake kutumia uwanja wa Craven Cottage kwa mechi zao za nyumbani kwa kipindi hicho.

Kwa taarifa hiyo inaeleza kwamba sehemu kubwa ya mechi za Ligi Kuu England zitachezwa uwanjani Craven Cottage.

Lakini, mechi za Ligi ya Mabingwa Ulaya na zile za upinzani mkali kama za kukabiliana na vigogo wenzao wa Big Six zitapigwa ama Wembley au Twickenham.

Chelsea imekifuata pia chama cha mchezo wa rugby, ambacho wamepanga kuutumia uwanja wao wa Twickenham kwenye mechi za mashindano mengine nje ya rugby na hilo linawafanya mabosi wa The Blues kwenda kupeleka maombi yao huko.

Chama hicho cha Rugby kinataka kuutumia uwanja wao wa Twickenham kama sehemu ya kuwaingizia mapato ili kutimiza mpango wao wa kuufanyia marekebisho uwanja wa taifa wa mchezo huo wa rugby.

Craven Cottage upo umbali wa maili 1.6 tu kutoka Stamford Bridge, lakini uwezo wake ni kuingiza watazamaji 29,600 wakati marekabisho yake yatakapokamilika majira ya yajayo ya kiangazi.

Twickenham inaingiza watazamaji 82,000, wakati Wembley watazamaji 90,000

Mechi za Chelsea zilizobaki kwenye Ligi kuu msimu huu

-Aprili 1 vs Aston Villa (nyumbani)

-Aprili 4 vs Liverpool (ugenini)

-Aprili 8 vs Wolves (ugenini)

-Aprili 15 vs Brighton (nyumbani)

-Aprili 22 vs Man United (ugenini)

-Aprili 26 vs Brentford (nyumbani)

-Aprili 29 vs Arsenal (ugenini)

-Mei 6 vs Bournemouth (ugenini)

-Mei 13 vs Nottm Forest (nyumbani)

-Mei 20 vs Man City (ugenini)

-Mei 28 vs Newcastle (nyumbani)