Chelsea, Gittens bado kidogo

Muktasari:
- Matajiri hao wa Jiji la London, tayari wameanza mapema sana dirisha la usajili na mbali ya mastaa Estevao Willian anatarajiwa kujiunga rasmi kutoka Palmeiras, sambamba na chipukizi wa Ecuador Kendry Paez ambao walisajiliwa kabla ya dirisha hili, pia imeshakamilisha usajili wa Liam Delap kutoka Ipswich na Dario Essugo kutoka Sporting Lisbon wiki iliyopita.
LONDON, ENGLAND: CHELSEA imefikia hatua nzuri ya kumsajili nyota wa Borussia Dortmund, Jamie Gittens ambaye atakuwa mchezaji wao wa tano dirisha hili la usajili la majira ya kiangazi, ikiwa ni katika harakati za kujiandaa na msimu mpya na wa mashindano ya Kombe la Dunia la Klabu.
Matajiri hao wa Jiji la London, tayari wameanza mapema sana dirisha la usajili na mbali ya mastaa Estevao Willian anatarajiwa kujiunga rasmi kutoka Palmeiras, sambamba na chipukizi wa Ecuador Kendry Paez ambao walisajiliwa kabla ya dirisha hili, pia imeshakamilisha usajili wa Liam Delap kutoka Ipswich na Dario Essugo kutoka Sporting Lisbon wiki iliyopita.
Chelsea imewasilisha ofa ya Pauni 29.5 milioni kwa ajili ya Gittens lakini inaaminika Dortmund itataka kiasi kikubwa zaidi, lakini lengo la Chelsea ni kukamilisha dili hilo kabla ya dirisha la kwanza la usajili kufungwa Jumanne.
Gittens, ambaye ni mchezaji wa timu ya taifa ya England chini ya miaka 21, aliwahi kuichezea akademia ya Chelsea akiwa mdogo kabla ya kuondoka kujiunga na Manchester City, lakini akaondoka mwaka 2020 na kuhamia Bundesliga, akijiunga na Dortmund. Tangu wakati huo amekuwa na mafanikio, akicheza mechi zaidi ya 100 na kufunga mabao 17 na 12 yalikuwa ni yale ya msimu uliopita.
Ingawa bado ana miaka mitatu kwenye mkataba wake, inaonekana yuko karibu kuondoka Dortmund endapo timu hizo mbili zitakubaliana juu ya ada ya uhamisho.
Mkataba wake una kipengele cha Dortmund kumwachia kwa Pauni 50 milioni, lakini Chelsea inataka kutoa chini ya hapo.
Mkurugenzi wa michezo wa Dortmund, Sebastian Kehl alikiri mapema mwaka huu kuna klabu zinazomfuatilia Gittens;
"Ndiyo kuna timu zinamhitaji. Ni mchezaji mzuri. Tutakuwa na mazungumzo hivi karibuni. Kama tutapokea ofa, itabidi tuzifanyie kazi. Tunataka kupunguza matumizi ya mishahara. Hivyo inawezekana wachezaji wengine wakaondoka kwenye kikosi chetu msimu ujao."
Ikiwa Chelsea itafanikisha dili hilo, Gittens anatarajiwa kuwa mbadala wa Jadon Sancho, ambaye ameondoka baada ya timu hiyo kuamua kutotumia kipengele cha kulipa Pauni 25 milioni ili kumnunua moja kwa moja na badala yake wamelia Pauni 5 milioni ili kumrudisha Manchester United.