Carragher amshangaa Sancho anavyokaba
Muktasari:
- Winga huyo anayekipiga kwa mkopo Chelsea akitokea Manchester United aliingia uwanjani kuchukua nafasi ya majeruhi Noni Madueke kipindi cha kwanza katika mechi ya Ligi Kuu England iliyofanyika uwanjani Amex, juzi Ijumaa.
LONDON, ENGLAND: JAMIE Carragher amemchana Jadon Sancho kwa kushindwa kuonyesha jitihada kuinusuru Chelsea isikumbane na udhalilishaji kutoka kwa Brighton.
Winga huyo anayekipiga kwa mkopo Chelsea akitokea Manchester United aliingia uwanjani kuchukua nafasi ya majeruhi Noni Madueke kipindi cha kwanza katika mechi ya Ligi Kuu England iliyofanyika uwanjani Amex, juzi Ijumaa.
Sancho hakufanya chochote cha maana kwenye mechi hiyo na kukifanya kikosi cha kocha Enzo Maresca kikikumbana na udhalilishaji mkubwa baada ya kuchapwa mabao 3-0 huku kikiwa na mashuti sifuri yaliyolenga golini.
Lakini, ukabaji wa Sancho ndiyo uliowashangaza wengi akiwamo Carragher, ambaye alikuwa akichambua mechi hiyo kupitia Sky Sports. Winga huyo wa zamani wa Borussia Dortmund alishindwa kumkaba Yankuba Minteh asifunge bao jingine wakati Chelsea ikiwa nyuma 2-0.
Minteh aliweza kumhadaa Sancho ndani ya boksi na kuifungia Brighton bao la tatu, huku winga huyo wa England akibaki amesimama tu anashangaa kama ameibiwa simu kwenye mataa.
Carragher alisema: “Hebu mtazame Sancho na Minteh, anafanya nini huyu mtu? Sawa, Minteh ana kiwango cha kuwa staa, lakini si kwa ukabaji ule wa Cucurella na Sancho, hovyo sana. Ule ulikuwa usiku mbaya sana kwa Enzo Maresca na Chelsea.”
Siku chache zilizopita Sancho aliwachukiza mashabiki wa Man United baada ya kuipiga kijembe timu yao kufuatia Marcus Rashford kwenda Aston Villa, alipokomenti neno “Uhuru” mtandaoni.
Na hapo, mashabiki wa Man United wakapata la kusema: “Carragher amepiga ngumi za maana! Hii ni sawasawa kabiwa kwa Sancho.” Mwingine alisema: “Ametoweka kabisa, ameshindwa kumkaba mtu wake, akafanya ubao usomeke 3-0. Carragher umemaliza.”
Shabiki wa tatu alisema: “Carragher ameuliza Sancho anaenda wapi??? Tulikuwa tukijiuliza mara nyingi sana swali kama hilo. Sasa Chelsea nao wanaona kwanini tulitaka aondoke.”
Na shabiki wa nne alisema: “Sancho alikuwa anafurahia ‘uhuru’ akamwacha Mintah aende zake.”