Carragher amkalia kooni Conte atimuliwe

LONDON, ENGLAND . MKONGWE wa soka Jamie Carragher, ameushinikiza uongozi wa Tottenham Hotspurs umtimue kocha wa timu hiyo Antonio Conte kufuatia kauli mbovu alizotoa Antonio Conte.

Kauli hiyo aliisema baada ya Spurs kulazimishwa sare ya mabao 3-3 dhidi ya Southampton kwenye mechi ya Ligi Kuu England huku Conte akiwaponda wachezaji wake.

Beki huyo zamani wa Liverpool alishangazwa na matokeo hayo akisisitiza uwamuzi ufanyike haraka ili wainusuru timu hiyo ambayo imepoteza mvuto kwasasa.

Spurs iliyokuwa mbele kwa mabao 3-0 ilijikuta inaangukia pua dhidi ya Southampton inayopambana kutoshuka daraja msimu huu, lakini Carragher akadai huo ni uzembe.

Carragher aliibuka na kuandika maneno ya kuwashinikiza mabosi wa Spurs kimtindo kupitia akaunti yake ya Twitter kwamba Conte anachotaka ni kufukuzwa kazi kufuatia kauli aliyozungumza baada ya mchezo huo.

"Conte anachotaka ni kufukuzwa kazini kabla mechi za kimataifa, Spurs wafanye maamuzi haraka iwezekanavyo" baadaye akajibu swali alipoulizwa na nyota wa zamani wa Watford Troy Deeney kufuatia maneno ya Conte: "Kauli zake kuhusu klabu sio nzuri, ni kweli Spurs haijawahi kubeba taji lolote kwa muda mrefu, lakini kuizungumzia vibaya timu yako nadhani amekosea, analipwa pesa nyingi na mabosi wake halafu unaongea vitu kama hivyo,"

Conte aliwajia juu wachezaji wake baada ya sare ya kushtukiza waliopata akidai wachezaji wake hawajitumi kwasababu hawaoni umuhimu wa mechi wanazocheza.

"Wamezoea kucheza hivyo, hawajitumi, hawataki kucheza kwa presha, wanachukulia kawaida sana, hii ndio stori ya Tottenham kila siku,niliwaambia nataka kuona wachezaji wakijituma lakini hakuna, wachezaji waonyeshe upambanaji wao sio tu mazoezini" alisema Conte kwa hasira

Wakati huo huo fowadi wao Richarlison aliondoka uwanjani akiwa anabubujikwa machozi baada ya kuumia mapema wakati mchezo wao dhidi ya Southampton ukiendelea huku akibembelezwa na Conte.