Cape Verde yatangulia 16 bora ikimsubiri Salah

CAPE Verde imekuwa timu ya kwanza kufuzu hatua ya 16 bora ya Fainali za Afcon, mwaka huu zinazofanyika Ivory Coast, ikiwa ni mara ya pili kwenye historia yao.
Timu hii ambayo ipo kundi B imefuzu baada ya kufikisha pointi sita ambazo hakuna timu yoyote inayoweza kuzifikia ikijihakikisha kumaliza kileleni juu ya mabingwa mara 7 wa Afcon, Misri na mabingwa mara nne, Ghana.
Pointi hizo imezipata baada ya kushinda mechi mbili, ikiwemo mchezo wa leo dhidi ya Msumbiji ikishinda mabao 3-0 baada ya ushindi kwenye mechi ya kwanza wa mabao 2-1 dhidi ya Ghana.
Mara ya kwanza kushiriki fainali hizi ni mwaka 2013 na ilitinga robo fainali na kutolewa na Ghana kwa kipigo cha mabao 2-0.
Ilishiriki tena mwaka 2015 lakini ikaishia hatua ya makundi kabla ya kurudi mwaka 2021 na ilishia hatua ya 16 bora baada ya kufungwa na Senegal mabao 2-0.