Cantona ambabua tajiri Man United
Muktasari:
- Gwiji huyo wa Man United , amefichua kuwa mmiliki wa klabu hiyo, Sir Jim Ratcliffe, alikataa msaada wake. “Hakuonekana kuwa na nia…”
UNAMKUMBUKA nyota wa kifaransa aliyeweka heshima kubwa Manchester United? Eric Cantona, ndiye aliyekusudiwa hapa. Sasa jamaa huyo ameamua kumlipua bilionea wa klabu hiyo ya England. Sir Jim Ratcliffe, akisema alikataa msaada wake Man United.
Gwiji huyo wa Man United , amefichua kuwa mmiliki wa klabu hiyo, Sir Jim Ratcliffe, alikataa msaada wake. “Hakuonekana kuwa na nia…”
Aprili mwaka huu, Cantona alisema kwamba Ratcliffe alikuwa “akiitoa roho” ya klabu na kudai kwamba asingechagua kuishabikia United sasa mradi Ratcliffe ndiye yuko mamlakani.
Mfaransa huyo, ambaye alichezea United mara 185 kati ya 1992 na 1997, anajulikana kwa kuwa na maoni makali na hasiti kusema anachokiamini kuhusu klabu yake ya zamani, ambayo anadai ina tatizo kubwa katika ngazi ya juu ya uongozi chini ya Ratcliffe.
“Naiunga mkono United kwa sababu naipenda sana, lakini sasa kama ningekuwa shabiki ambaye anatakiwa kuchagua klabu, sidhani kama ningechagua United,” Cantona alisema katika hafla ya FC United, klabu iliyoundwa baada ya ununuzi wa Glazer mwaka 2005.
“Kwa sababu sijisikii karibu na aina hizi za maamuzi. Wana mkakati mwingine, mradi mwingine. Je, unajiona karibu na mradi huu? Sidhani.”
Ratcliffe akataa msaada wa Cantona
Sasa kiungo huyo wa zamani amezungumza tena, akielekeza lawama kwa Ratcliffe baada ya kukataa msaada wake kwa kipindi cha miaka michache iliyopita.
“Nina shauku na miradi mingine mingi, lakini nilifikiri kwamba kwa miaka miwili au mitatu ningeweza kuiweka pembeni na kujaribu kutoa kitu kwa klabu hii, ambayo imenipa kila kitu.
“Lakini hakonekana kuwa na nia. Nilifanya kilichonihusu, hivyo sijihisi na hatia tena. Nilijaribu kadiri ya uwezo wangu.
“Sir Alex Ferguson alitengeneza mtindo wa soka la kushambulia kwa kuvutia, ambao wamiliki wapya walipaswa kuuendeleza. Badala yake, wameuharibu.”
Ratcliffe amekosolewa kutokana na hatua zake za kupunguza gharama ambazo zilisababisha takriban wafanyakazi 450 kupoteza ajira na kuondolewa kwa baadhi ya huduma kama chakula cha bei nafuu kwenye mgahawa wa klabu. Hivyo, Cantona anaonekana wazi kutomkubali bilionea huyo ambaye, licha ya United kuwa katika kiwango kizuri kwa sasa, bado ni mtu mwenye utata mkubwa.