Bye Bye Ramos, PSG, Manchester United zaanza kumtolea macho

Muktasari:

BAADA ya miaka 16 ya mafanikio na historia ya kipekee, nahodha na beki wa kisiki wa Real Madrid, Sergio Ramos ameachana rasmi na timu hiyo baada ya kushindwa kufikia makubaliano juu ya mkataba mpya.

MADRID, HISPANIA. BAADA ya miaka 16 ya mafanikio na historia ya kipekee, nahodha na beki wa kisiki wa Real Madrid, Sergio Ramos ameachana rasmi na timu hiyo baada ya kushindwa kufikia makubaliano juu ya mkataba mpya.

Mkataba wa beki huyo mwenye umri wa miaka 35 na Real Madrid unamalizika mwishoni mwa mwezi huu na vikao vya majadiliano baina ya pande hizo mbili kuurefusha mkataba vimeonekana kutozaa matunda.

Real Madrid ilipanga kumuongeza mkataba wa mwaka mmoja Ramos na kumkata asilimia 10 ya mshahara anaopata sasa ili iendelee kubaki naye lakini upande wa Ramos unaonekana kutokubaliana na mapendekezo hayo.

Inatajwa kuwa Ramos yeye anataka apewe mkataba wa miaka miwili na kulipwa mshahara sawa na ule anaolipwa katika mkataba wa sasa jambo ambalo upande wa Real Madrid umeonekana kushindwa kulimudu.

Taarifa iliyotolewa na klabu ya Real Madrid imethibitisha kuachana na beki huyo na jana alitegemewa kuaga rasmi kupitia mkutano na waandishi wa habari.

“Real Madrid inatangaza kuwa kesho, Alhamisi, Juni 17 saa 6.30 mchana kutakuwa na tukio la heshima na kumuaga nahodha wetu Sergio Ramos ambalo litahudhuriwa na Rais Florentino Perez. Sergio Ramos baada ya hapo atazungumza na vyombo vya habari,” imesema taarifa hiyo ya Real Madrid.

Taarifa hiyo inaamanisha kuwa mchezo wa marudiano ugenini wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Chelsea waliofungwa kwa mabao 2-0 mwezi uliopita, ndio ulikuwa wa mwisho kwa Ramos kuitumikia Real Madrid.

Ramos alijiunga na Real Madrid mwaka 2005 akitokea Sevilla na tangu hapo amepata mafanikio makubwa akiwa na jezi za timu hiyo kutokana na idadi kubwa ya mataji aliyoshinda akiwa na kikosi hicho.

Katika kipindi hicho chote, Ramos ametwaa jumla ya mataji 22 yaliyoambatana na tuzo nyingi binafsi.

Akiwa na Real Madrid, Ramos ametwaa mataji manne ya Klabu Bingwa ya Dunia, Mataji manne ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Uefa Super Cup mara tatu, Taji la Supercopa de Espana mara nne, Copa del Rey mara mbili na lile la Ligi Kuu ya Hispania mara tano.

Mfano wa tuzo binafsi alizopata ni ile ya mlinzi bora wa Ligi Kuu ya Hispania aliyotwaa mara tano, mlinzi bora wa Uefa mara mbili, mchezaji bora wa klabu bingwa ya dunia mara moja na kuingia katika kikosi bora cha Uefa mara tisa.