Burnley yashuka daraja, Spurs yaamsha matumaini ya kucheza Ulaya

Muktasari:

  • Burnley inayonolewa na Vincent Kompany imeshindwa kupambana kwenye ligi baada ya kuvuna pointi 24 katika mechi 37.

LONDON, ENGLAND: TIMU ya Burnley imeshuka daraja baada ya kudumu kwa msimu mmoja tu kwenye Ligi Kuu England na kwamba msimu ujao itakuwa kwenye Championship baada kukubali kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Tottenham Hotspur katika mchezo wa Ligi Kuu uliofanyika Jumamosi.

Burnley inayonolewa na Vincent Kompany imeshindwa kupambana kwenye ligi baada ya kuvuna pointi 24 katika mechi 37.

Burnley ilihitaji kushinda mchezo huo ili kufufua matumaini ya kubaki Ligi Kuu England, lakini sasa kipigo kimetibua mipango, hivyo hata kama itashinda mechi ya mwisho iliyobaki, haitasaidia kitu.

Burnley chini ya Kompany ilipanda daraja kibabe mwaka jana, lakini presha kwenye Ligi Kuu England imekuwa kubwa kwao na hivyo imerejea kwenye Championship.

Huu ulikuwa msimu wa tisa kwa Burnley kwenye Ligi Kuu England, ambapo mara yao ya kwanza ilikuwa msimu wa 2009-10 ambapo ilipanda na kushuka kisha ikarudi tena msimu wa 2014-15 na ikashuka tena baada ya msimu mmoja. Ikacheza Championship kwa msimu mmoja kisha ikarejea tena 2016-17, ikadumu katika EPL kwa misimu sita kabla ya kushuka 2021-22 ambapo ilimaliza ya tatu kutoka mkiani. Mwaka jana ilibeba taji la Championship na kupanda Ligi Kuu England msimu huu,  lakini imeshuka tena na msimu wa 2024-25 itacheza kwenye Championship.

Hata hivyo, licha ya matokeo mabaya ambayo timu hii imeyapata msimu huu, matajiri wa Burnley wanaripotiwa kuwa na imani na kocha wao Kompany na wamepanga kuendelea naye.

Ushindi ambao Spurs kaatika mchezo huu umewafanya kujiweka katika mazingira mazuri ya kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao ikiwa inashika nafasi ya tano kwa pointi 63, huku Aston Villa iliyo nafasi ya nne ikiwa na pointi 67, hivyo kama Spurs ikichanga karata zake vizuri inaweza kuwashusha vijana hao wa Unai Emery katika mechi mbili zilizobaki.