Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Burnley yaendeleza rekodi ya panda shuka Premier League

Muktasari:

  • Kushuka kwa Burnley kunatokana na pointi 20 ilizonazo, hata ikishinda mechi nne zilizobaki, maana yake itamaliza msimu na pointi 32 ambazo hivi sasa zimepitwa na West Ham United iliyopo nafasi ya 17, nje ya mstari wa kushuka daraja. West Ham inazo 33.

KICHAPO cha bao 1-0 ilichopokea Burnley usiku wa Aprili 22, 2026 kutoka kwa Manchester City, kimehitimisha safari ya timu hiyo kuendelea kuwepo ndani ya Premier msimu ujao, huku ikiungana na Wolverhampton iliyoshuka Jumatatu wiki hii.

Kushuka kwa Burnley kunatokana na pointi 20 ilizonazo, hata ikishinda mechi nne zilizobaki, maana yake itamaliza msimu na pointi 32 ambazo hivi sasa zimepitwa na West Ham United iliyopo nafasi ya 17, nje ya mstari wa kushuka daraja. West Ham inazo 33.

Hata hivyo, kushuka kwa Burnley hata wao wenyewe hawajashtuka sana huku kocha wa kikosi hicho, Scott Parker akisema: "Haitanishangaza tukirudi Premier baada ya msimu ujao."

Kauli hiyo ya Parker hajaitoa kwa bahati mbaya, bali ameangalia rekodi ya maajabu iliyonayo Burnley ambayo ni kama imezoea kupanda na kushuka.

Burnley imejithibitisha rasmi kuwa wafalme wa kupanda na kushuka nchini Uingereza kufuatia kushuka kwao daraja kutoka Ligi Kuu (Premier League).

Kipigo hicho cha 1-0 dhidi ya Manchester City, imewafanya Burnley kutumia msimu wa tano mfululizo wakizunguka kati ya madaraja mawili ya juu ya soka la Uingereza.

Tangu mwaka 1992, Burnley wamekuwa na rekodi ya kupanda daraja mara nane na kushuka mara sita, takwimu zinazowafanya kuwa miongoni mwa timu zenye mabadiliko mengi zaidi ya daraja nchini humo.

Rekodi zinaonyesha kuwa, Burnley wameingia kwenye mzunguko wa kipekee tangu msimu wa 2021-22.

Katika msimu huo, walishuka daraja wakiwa nafasi ya 18 na pointi 35. Hata hivyo, walirejea kwa kishindo msimu uliofuata wa 2022-23 kwa kushinda ubingwa wa Championship wakiwa na pointi 101.

Furaha hiyo haikudumu, kwani msimu wa 2023-24 walishuka tena wakiwa na pointi 24 tu. Mzunguko huu uliendelea msimu wa 2024-25 ambapo walipanda tena kwa pointi 100, kabla ya kushuka tena msimu huu wa 2025-26 wakiwa na pointi 20 tu na michezo minne kusalia.

Ni klabu ya Fulham pekee, kati ya mwaka 2017 na 2022, iliyowahi kufikia rekodi hii ya panda shuka kwa miaka mitano mfululizo.

Mabadiliko ya falsafa ya klabu hiyo, yametajwa kuchangia pakubwa katika hali hii. Chini ya kocha Sean Dyche, Burnley walikuwa na utulivu mkubwa, wakicheza Ligi Kuu kwa misimu sita kati ya nane. Dyche aliweza hata kuifikisha timu hiyo kwenye mashindano ya Ulaya akitumia wachezaji wenye tabia ngumu na bajeti ndogo.

Hata hivyo, baada ya kufutwa kazi kwa Dyche mnamo Aprili 2022, klabu ilianza mchakato wa kubadili utambulisho wake.

Vincent Kompany alichukua mikoba na kubadili kabisa mtindo wa uchezaji, akileta soka la kisasa na kusajili wachezaji wengi vijana na wa kigeni, jambo ambalo lilikuwa geni kwa utamaduni wa Burnley. Ingawa alifanikiwa kupandisha timu, lakini alishindwa kuibakiza Ligi Kuu na kisha kuondoka kwenda Bayern Munich.

Scott Parker, kocha wa sasa, ana rekodi ya kipekee ya kupandisha timu kila anapokuwa Championship (akiwa amefanya hivyo na Fulham, Bournemouth, na sasa Burnley), lakini hajawahi kufanikiwa kuibakiza timu yoyote Ligi Kuu kama meneja.

Moja ya sababu iliyotajwa kuibeba Burnley inaposhuka daraja kushiriki Championship na kurudi haraka Premier ni mfumo wa "parachute payments". Haya ni malipo ya mgao wa kifedha unaofanywa na Premier kwa klabu zilizoshuka daraja ili kuzisaidia kuzoea mapato yaliyopunguza kwani kiwango cha fedha kwa Premier na Championship ni tofauti.

Glen Little, mchezaji wa zamani wa Burnley, anabainisha kuwa, malipo haya yanawapa Burnley faida kubwa ya kifedha wanaposhuka daraja na kujiimarisha zaidi.

Katika misimu mitano iliyopita, timu mbili kati ya tatu zilizopanda kutoka Championship zilikuwa zikipokea malipo haya. Hali hii inatengeneza pengo kubwa kati ya timu zinazoshuka kutoka Premier na nyingine ndogo za Championship ambazo hazipo vizuri kiuchumi.

Licha ya mafanikio ya kupanda daraja mara kwa mara, mashabiki wa Burnley hawaonyeshi kufurahishwa na hali ya sasa.

Natalie Bromley, mwandishi na shabiki wa Burnley, anaelezea klabu hiyo kama isiyo na kitu na iliyopoteza utambulisho wake wa kihistoria wa "grit" ya East Lancashire ambayo imekuwepo tangu 1882.

Glen Little anaongeza kuwa, ingawa timu imekuwa na bahati mbaya na maamuzi ya VAR msimu huu, kuna hofu kuwa wachezaji wamepoteza morali na kocha amekosa mbinu mpya.

Baada ya kushuka, Burnley sasa wanakabiliwa na changamoto ya jinsi ya kuvunja mzunguko huu.

Wakati wanatarajiwa kupanda tena msimu ujao kutokana na ubora wa kikosi chao, swali linabaki: Je, wataweza kusajili wachezaji sahihi watakaowawezesha kubaki Premier wakirejea?

Burnley wanabaki kuwa timu inayofurahia maisha ya ubingwa wa Championship, lakini inayoteseka kukabiliana na vigogo wa Premier.

Kwa sasa, Rotherham United ndio timu pekee nchini Uingereza yenye mabadiliko mengi zaidi ya daraja (16) kuliko Burnley (14) tangu kuanzishwa kwa Premier League.