Bruno: Ronaldo atatupa ndoo

Friday September 10 2021
bruno pic

MANCHESTER, ENGLAND. KIUNGO wa Manchester United, Mreno, Bruno Fernandes, anaamini ujio wa Cristiano Ronaldo Manchester United, utaleta chachu kwenye mbio za kuwania ubingwa msimu huu wa Ligi Kuu England na mataji mengine.

Bruno ameendelea kuwa mchezaji tegemeo kwenye kikosi cha Man United tangu aliposajiliwa akitokea Sporting Lisbon na mreno huyo tangu alipotua Man United mwaka 2020, kwenye dirisha dogo la usajili mwezi Januari, amefikisha jumla ya mabao 43 katika mechi 83 alizocheza katika mashandano yote, huku pia atoa asisti 25.

Aidha, Bruno alisema wachezaji wenzie wanajivunia uwepo wa Ronaldo, kutokana na uwezo wake wa kufumania nyavu na tamaa ya kupata mafanikio kwa muda wote anapokuwa uwanjani.

Man United haijashinda taji lolote tangu 2017 ilipotwaa ubingwa wa Europa League chini ya Jose Mourinho.

Hata hivyo, Bruno, 27, anafahamu mafanikio ya Ronaldo tangu alipokuwa akikipiga Old Trafford na kubeba mataji 33, ambayo alishinda akiwa na timu zote tatu Man United, Real Madrid na Juventus, alizowahi kuzichezea.

Bruno alitema cheche akisisitiza kila mtu kwenye viunga vya Old Trafford, ana furaha kubwa na kujiamini baada ya kurejea kwa staa huyo aliyewahi kuzinyanyasa timu pinzani za Ligi Kuu England.

Advertisement

“Mambo yatakuwa shwari tu, kila mtu anafahamu balaa lake, nina imani ataongeza kitu, kila mmoja ana furaha. Hata wachezaji tunafahamu kweli tumepata kifaa hasa,” alisema Bruno.

Ronaldo, 36, aliondoka Man United kutua Real Madrid 2009, kisha Juventus kabla ya kurejea United katika dirisha hili.

Advertisement
​