Bruno Fernandes, Cristiano Ronaldo ngoma droo
Muktasari:
- Ushahidi wa hilo ni tuzo yake ya hivi karibuni ya Mchezaji Bora wa Mwezi wa Ligi Kuu England kwa mwezi Machi nasasa ameshinda mara sita tangu ajiunge na Mashetani Wekundu 2020.
MANCHESTER, ENGLAND: KIUNGO wa kimataifa wa Ureno, Bruno Fernandes anaendelea kudhihirisha ni mmoja wa wachezaji muhimu kwenye kikosi cha Manchester United, huku jina lake likiendelea kuandikwa katika historia ya soka la England.
Ushahidi wa hilo ni tuzo yake ya hivi karibuni ya Mchezaji Bora wa Mwezi wa Ligi Kuu England kwa mwezi Machi nasasa ameshinda mara sita tangu ajiunge na Mashetani Wekundu 2020.
Mafanikio hayo yanaonyesha namna alivyo na athari kubwa uwanjani tangu alipowasili klabuni hapo na zaidi ya hapo, amefikia rekodi iliyowekwa na nyota wa zamani wa klabu hiyo, Cristiano Ronaldo.
Tangu ajiunge na Man United Januari 2020, Bruno amekuwa kiungo mshambuliaji mwenye mchango mkubwa akiwa amefunga zaidi ya mabao 100 na kutoa pasi nyingi za mabao katika mashindano yote akiongoza kutengeneza nafasi na kuchangia mabao tangu alipocheza mechi yake ya kwanza, huku pia akifunga zaidi ya mabao 10 katika kila msimu tangu atue.
AIFIKIA REKODI YA CRISTIANO RONALDO
Ronaldo alishinda tuzo ya mchezaji bora mara sita akiwa Man United na sasa Bruno ambaye pia ni mwenzake katika timu ya taifa ya Ureno, ameifikia idadi hiyo. Hatua hiyo inamuweka Bruno katika kundi la wachezaji wachache waliowahi kufikia kiwango hicho, akishirikia rekodi na mmoja wa magwiji wakubwa wa soka duniani.
Bruno alishinda tuzo yake ya kwanza Februari 2020, mwezi wake wa kwanza tu katika ligi hiyo. Baadaye alishinda Juni, Novemba na Desemba, mwaka huo huo akiwa mchezaji wa kwanza katika historia ya ligi hiyo kushinda mara nne ndani ya mwaka mmoja. Pia alishinda tena Machi, mwaka jana na sasa ameongeza nyingine 2026.
Kwa sasa, nyota huyo mwenye umri wa miaka 31 amemzidi nguli wa klabu, Wayne Rooney, aliyekuwa na tuzo tano, na sasa ana nafasi ya kuvunja rekodi ya muda wote. Wachezaji kama Harry Kane, Sergio Agüero na Mohamed Salah wana tuzo saba kila mmoja.
Kwa kuwa Bruno ana mkataba hadi Juni 2027 (ukiwa na chaguo la kuongeza mwaka mmoja zaidi), ana nafasi kubwa ya kufikia au hata kuvunja rekodi hiyo. Hadi mwanzoni mwa Aprili 2026, Bruno amecheza zaidi ya mechi 300.
UWANJANI SASA
Mbali na tuzo binafsi, mchango wake katika kikosi cha Man United ni mkubwa na msimu huu ametoa asisti 16, akivunja rekodi ya David Beckham aliyeondoka akiwa nazo 15. Kwa sasa anasikilizia asisti nne tu kufikia rekodi ya kuwa nazo 20 inayoshikiliwa na Thierry Henry na Kevin De Bruyne ambao wanazo nyingi zaidi katika msimu mmoja.
Katika kikosi cha Man United inayotaka kurejea kileleni mwa soka la Ulaya, Bruno siyo tu kafikia rekodi ya Ronaldo, bali analenga kumpita na kutengeneza ufalme wake binafsi katika Uwanja wa Old Trafford.
TAKWIMU ZA BRUNO MAN UNITED MASHINDANO YOTE
2024/25: Mechi 36+, mabao 8+, asisti 10+
2023/24: Mechi 35+, mabao 10+, asisti 8+
2022/23: Mechi 37+, mabao 8+, asisti 8+
2021/22: Mechi 36+, mabao 10+, asisti 6+
2020/21: Mechi 37+, mabao 18+, asisti 12+
2019/20: Mechi 14+, mabao 8+, asisti 7+
NNE ZIJAZO ZA MAN UNITED
vs Leeds United, Aprili 13 (Old Trafford)
vs Chelsea, Aprili 18 (Stamford Bridge)
vs Brentford, Aprili 27 (Old Trafford)
vs Liverpool, Mei 2 (Old Trafford)