Bruno aisubirisha Man United
Muktasari:
- Mkataba wa sasa wa raia huyo wa Ureno na United unatarajiwa kumalizika mwaka 2027, ukiwa na kipengele cha kuongezewa mwaka mmoja zaidi.
KIUNGO na nahodha wa Manchester United, Bruno Fernandes, 31, amepanga kusubiri hadi mwisho wa msimu huu kabla ya kufanya uamuzi juu ya mustakabali wake ikiwa ataendelea kuwepo katika kikosi hicho au ataondoka.
Mkataba wa sasa wa raia huyo wa Ureno na United unatarajiwa kumalizika mwaka 2027, ukiwa na kipengele cha kuongezewa mwaka mmoja zaidi.
Fernandes ameendelea kuwa mhimili muhimu katika kikosi cha kwanza cha Old Trafford, lakini mustakabali wake bado unaendelea kuwa na sintofahamu, huku baadhi ya taarifa zikidai Man United imempa muda kabla ya kuanza kwa michuano ya Kombe la Dunia mwaka huu kuw awe ameshafanya uamuzi.
Al-Hilal ya Saudi Arabia ni miongoni mwa timu zinazohitaji saini ya fundi huyu na iliwasilisha ofa kwa ajili ya kumsajili tangu dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana lakini Bruno mwenyewe alikataa kuondoka na kusisitiza bado anahitaji kuendeela kucheza soka la kiushindani licha ya mabosi wa mashetani hao wekundu kuwa tayari kumpiga bei.
Tangu kuanza kwa msimu huu, Bruno amecheza mechi 22 za michuano yote na kutoa asisti 11.
Jean-Philippe Mateta
NOTTINGHAM Forest imewasilisha ofa ya Pauni 35 milioni kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji wa Crystal Palace na timu ya taifa ya Ufaransa, Jean-Philippe Mateta mwenye umri wa miaka 28. Hata hivyo, Palace imesisitiza inahitaji ofa isiyopungua Pauni 40 milioni ili kumruhusu mchezaji huyo kuondoka. Klabu hiyo ya London pia imeweka sharti la kumpata mbadala kabla ya kukubali ofa yoyote, kutokana na umuhimu wa Mateta katika safu yao ya ushambuliaji. Mazungumzo yanaendelea, lakini Palace hawako tayari kushusha bei kwa sasa.
Beto
JUVENTUS inamchunguza mshambuliaji wa Everton na Guinea-Bissau, Beto, 27, kama sehemu ya mastaa inayohitaji kuwasajili ili kuimarisha safu yao ya ushambuliaji dirisha la usajili la majira ya baridi. Everton bado haijaonyesha wazi kama iko tayari kumwachia staa huyu, lakini ofa itakayokidhi mahitaji yao inaweza kufungua mlango wa mazungumzo. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwakani. Tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 26 za michuano yote.
Federico Chiesa
JUVENTUS imeongeza jina la winga wa Liverpool na timu ya taifa ya Italia, Federico Chiesa, 28, kwenye orodha ya wachezaji inaowafuatilia dirisha hili la usajili. Chiesa, ambaye aliwahi kung’ara akiwa Juventus kabla ya kuondoka, anatajwa kuwa mmoja wa chaguo linalopewa kipaumbele zaidi na benchi la ufundi la Liverpool dirisha hili. Uzoefu wake Serie A na uwezo wa kucheza pembeni unawavutia mabosi wa Bianconeri. Liverpool bado haijatoa msimamo rasmi kuhusu mustakabali wa nyota huyo.
Ederson
ATLETICO Madrid iko tayari kuanza mazungumzo na Atalanta kuhusu uwezekano wa kumsajili kiungo wa klabu hiyo na Brazil, Ederson, 26. Ederson amekuwa kwenye kiwango bora Serie A tangu msimu uliopita na timu nyingi zimeonyesha nia ya kumsajili. Kocha Diego Simeone anamwona staa huyu kama ingizo muhimu katika safu yake ya kiungo msimu ujao. Atalanta bado haijafungua mlango rasmi wa mazungumzo, lakini inatarajiwa kuhitaji kiasi kikubwa cha pesa.
Tim Iroegbunam
EVERTON imekataa ofa iliyowasilishwa na Lazio kwa ajili ya kumsajili kiungo wa timu hiyo na England, Tim Iroegbunam, 22. Klabu hiyo ya Ligi Kuu England inaamini thamani ya mchezaji huyo ni kubwa zaidi ya kile kilichotolewa na wababe hao wa Serie A. Iroegbunam bado anaonekana kuwa sehemu ya mipango ya Everton ya muda mrefu, lakini ofa kutoka Lazio inadaiwa kumshawishi staa huyu. Mazungumzo kwa sasa yamesimama na yanaweza kuendelea ikiwa Lazio itarejea mezani na ofa mpya nono zaidi.
Jamal Lascelles
NEWCASTLE United imemwambia beki wake wa England, Jamal Lascelles, 32, yuko huru kuondoka ikiwa ofa sahihi itawasilishwa mezani dirisha hili. Lascelles, ambaye amekuwa katika kikosi cha Newcastle kwa miaka mingi, anakabiliwa na ushindani mkali wa nafasi ya kucheza. Uongozi wa Newcastle uko tayari kusikiliza ofa kutoka kwa klabu zinazomhitaji. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu.
David Moller Wolfe
WOLVES imekataa ofa ya Pauni 6.9 milioni iliyowasilishwa na Roma kwa ajili ya kumsajili beki wao wa kushoto na Norway, David Moller Wolfe, 23. Klabu hiyo ya Ligi Kuu England imeweka wazi haiko tayari kumwachia mchezaji huyo kwa kiasi hicho, ikiamini thamani yake ni kubwa zaidi. Wolfe amekuwa mchezaji tegemeo katika kikosi cha kwanza cha kwanza Wolves na tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 16 za michuano yote. Roma inaweza kurejea tena mezani na ofa kubwa zaidi.