Bradley Barcola arudi kwenye rada za Arsenal
Muktasari:
- Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta, anatafuta kwa udi na uvumba washambuliaji wapya ili kuimarisha kikosi chake. Hii inatokana na changamoto za majeraha zinazomuandama nyota wake Bukayo Saka, pamoja na kiwango kisichoeleweka cha Gabriel Martinelli msimu huu.
KLABU ya Arsenal inaripotiwa kuongoza mbio za kumsajili winga machachari wa Paris Saint-Germain, Bradley Barcola, katika kipindi kijacho cha majira ya kiangazi. Hatua hii inakuja baada ya mazungumzo ya mkataba mpya kati ya mchezaji huyo na mabingwa hao wa Ufaransa kusitishwa kwa muda.
Barcola, ambaye amekuwa mmoja wa wachezaji wanaotazamwa kwa ukaribu nchini Ufaransa, aliisaidia PSG kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita, akifunga mabao 21. Licha ya kufunga mabao 12 msimu huu, mchezaji huyo amekuwa akikosa muda wa kutosha wa kucheza kutokana na ushindani mkali kutoka kwa Ousmane Dembele na Khvicha Kvaratskhelia.
Kwa mujibu wa ripoti kutoka gazeti la L’Equipe la Ufaransa, PSG ipo tayari kumuuza Barcola ili kupata fedha za kusajili mshambuliaji mpya. Ingawa mkataba wake wa sasa unaisha mwaka 2028, mazungumzo yote yamesitishwa mpaka baada ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Hatima ya uhamisho huu inatarajiwa kuwa ya kuvutia kwani PSG itachuana vikali na Arsenal yenyewe kwenye mchezo huo wa fainali utakaopigwa Mei 30, 2026 jijini Budapest, jambo linaloongeza msisimko mkubwa kabla ya dirisha la usajili kufunguliwa.
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta, anatafuta kwa udi na uvumba washambuliaji wapya ili kuimarisha kikosi chake. Hii inatokana na changamoto za majeraha zinazomuandama nyota wake Bukayo Saka, pamoja na kiwango kisichoeleweka cha Gabriel Martinelli msimu huu.
Wakati Arsenal ikionekana kuwa mbele katika usajili wa nyota huyo, Liverpool imejiondoa kwenye mbio hizo. Liverpool imeamua kuachana na Barcola kwa sababu inatafuta winga wa kulia, huku ikitaka kumpa nafasi kijana wao chipukizi, Rio Ngumoha, upande wa kushoto.
Hali ya Barcola ndani ya PSG pia imeingia dosari baada ya ripoti kufichua kuwa kocha Luis Enrique alikasirishwa na uamuzi wake uwanjani wakati wa ushindi wa 2-0 dhidi ya Lens. Barcola alitolewa wakati wa mapumziko na nafasi yake kuchukuliwa na Vitinha.
Tangu ajiunge na PSG akitokea Lyon mwaka 2023, winga huyo ameshacheza mechi 150 na kufunga mabao 38. Arsenal, ambayo ilimkosa mchezaji huyo msimu uliopita baada ya kuamua kubaki PSG, sasa inapewa nafasi kubwa zaidi ya kukamilisha usajili wake.