Arsenal yapania kumaliza kazi ya ubingwa dhidi ya Man City
Muktasari:
- Arsenal (79) wanaongoza ligi wakiwa pointi mbili mbele ya Man City (77) na wataweza kuongeza pengo hilo hadi pointi tano iwapo watashinda dhidi ya Burnley kwenye mchezo wa kesho, Jumatatu kwenye Uwanja wao wa nyumbani Emirates.
KOCHA wa Arsenal, Mikel Arteta, amewataka wachezaji wake kutumia nafasi walizonazo kumaliza kazi ya kutwaa mataji msimu huu huku vita ya ubingwa wa Ligi Kuu England ikiendelea kupamba moto dhidi ya Manchester City.
Arsenal (79) wanaongoza ligi wakiwa pointi mbili mbele ya Man City (77) na wataweza kuongeza pengo hilo hadi pointi tano iwapo watashinda dhidi ya Burnley kwenye mchezo wa kesho, Jumatatu kwenye Uwanja wao wa nyumbani Emirates.
Katika mazingira hayo, Arsenal wanaweza kutangazwa mabingwa iwapo Manchester City watapoteza au kupata sare dhidi ya Bournemouth katika mchezo wao unaofuata.
Arteta alisema kikosi chake kimekuwa na maendeleo makubwa katika misimu ya hivi karibuni, lakini bado kinahitaji hatua ya mwisho ya kuthibitisha ubora wao kwa kutwaa mataji.
“Tunapaswa kuchukua hatua ya mwisho ya kukamilisha kazi. Hiyo ndiyo nafasi tuliyonayo katika siku chache zijazo,” alisema Arteta.
Kocha huyo aliongeza kuwa Arsenal imejengwa kwa juhudi za muda mrefu tangu alipoingia 2019 huku akisisitiza mchango wa wachezaji, uongozi na mashabiki katika kufikia hatua hiyo.
Arteta alieleza kuwa mafanikio hayawezi kupatikana kwa urahisi kutokana na ushindani mkubwa uliopo kwenye Ligi Kuu England lakini akasisitiza kuwa timu yake sasa iko karibu zaidi na mafanikio makubwa.
Arsenal inaelezwa kuwa na changamoto ya majeruhi hasa katika nafasi ya beki wa kulia baada ya Ben White kuungana na Jurrien Timber kwenye wodi ya majeruhi, jambo linalomlazimu kocha huyo kutafuta suluhisho la haraka.
Hata hivyo, Arteta alisema atatumia mbinu mabadala katika kufanya maamuzi ya kikosi, akisisitiza kuwa kila mchezo unahitaji uamuzi sahihi kulingana na hali ya wakati huo.