Bosi kasema... Man United itasajili

Muktasari:
- Hali ya uchumi wa Man United ilikuwa ikiibua maswali mengi kama Amorim atasajili kuunda kikosi chake au atabaki na wachezaji waliopo.
MANCHESTER, ENGLAND: MKURUGENZI Mtendaji Mkuu wa Manchester United, Omar Berrada amesema kocha Ruben Amorim ameanza kujadiliana na mabosi wa klabu juu ya mipango ya dirisha lijalo la usajili wa majira ya kiangazi hivyo bosi huyo atakabidhiwa mkwanja wa kunasa mastaa wapya dirisha likifunguliwa.
Man United ipo kwenye hatari ya kumaliza nafasi za chini zaidi kwenye Ligi Kuu England katika kipindi hiki cha kocha Amorim kutokana na kushindwa kupata matokeo mazuri tangu alipochukua mikoba ya kuinoa miamba hiyo ya Old Trafford, Novemba mwaka jana.
Kutokana na hali ya uchumi ya klabu, ilikuwa ikitishia kwamba kocha Amorim atalazimika kufanya kazi na kikosi alichokirithi kutoka kwa mtangulizi wake Erik ten Hag, huku yeye akifanya usajili wa bei nafuu, Patrick Dorgu na Ayden Heaven aliowanasa kwenye dirisha la Januari.
Lakini, sasa bosi Berrada amethibitisha mabosi wa timu hiyo na kocha Amorim wanafanya kazi kwa ukaribu kwenye mpango wa usajili wa wachezaji wapya, akimaanisha kwamba mkurugenzi wa ufundi, Jason Wilcox na Amorim wanaweka mambo yao sawa kutambua nani aje.
Akizungumza kabla ya mchezo wa marudiano wa raundi ya 16 bora dhidi ya Real Sociedad kwenye Europa League, Berrada alisema: "Tumekuwa tukizungumza mara kwa mara na kocha Ruben (Amorim). Ruben ana uhusiano mzuri na Jason Wilcox. Wote wana mawazo yanayoshabihiana vile wanavyotaka timu icheze."
Hali ya uchumi wa Man United ilikuwa ikiibua maswali mengi kama Amorim atasajili kuunda kikosi chake au atabaki na wachezaji waliopo.
Lakini, kwa kauli ya bosi huyo ina maana kwamba United licha ya mipango ya kujenga uwanja mpya unaobeba mashabiki 100,000 bado Amorim atakuwa na pesa za kusajili wakali wapya iwe timu itafuzu michuano ya Ulaya au la.