Boris ataka fainali Uefa ipigwe Uingereza

Muktasari:

WAZIRI Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson amelitaka shirikisho la soka barani Ulaya 'Uefa’ kuhamishia fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwenda Uingereza ili kutoa nafasi ya mashabiki kwenda kuishuhudia uwanjani.

LONDON, ENGLAND. WAZIRI Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson amelitaka shirikisho la soka barani Ulaya 'Uefa’ kuhamishia fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwenda Uingereza ili kutoa nafasi ya mashabiki kwenda kuishuhudia uwanjani.

Mchezo huo umepangwa kufanyika kwenye nchi ya Uturuki ambayo imewekwa kwenye mstari mwekundu na Uingereza kama nchi yenye maambukizi ya virusi vya corona, hivyo mashabiki wa Chelsea na Manchester City watakaokwenda kushuhudia fainali hiyo watalamizika kuingia gharama nyingine za kujitenga hotelini kwa siku 10 watakaporejea kutoka Istanbul baada ya fainali hiyo ya Mei 29.

Waziri Mkuu Johnson aliambia SunSport: “Ligi ya Mabingwa Ulaya ni michuano mikubwa kabisa ya ngazi ya klabu kwenye soka la Ulaya. Na timu mbili za England zitacheza fainali, hivyo itakuwa aibu kubwa kama mashabiki watashindwa kwenda kuhudhuria.

“Itakuwa jambo zuri sana kama fainali itafanyika hapa. Nataka kuwasaidia mashabiki wa timu hizo zote mbili kupata fursa ya kwenda uwanjani kutazama fainali.”

Kiongozi huyo wa serikali ya Uingereza alisema mechi hiyo ikipigwa England, kutakuwa na uhakika wa mashabiki wapatao 15,000 kuhudhuria.

Vilevile fainali hiyo ikichezwa Uturuki, basi timu zitalazimika kujiweka karantini baada ya kurejea.