Bingwa AFCON 2025 kubeba Sh 24 Bilioni
Muktasari:
- Tanzania katika michuano hiyo imepangwa Kundi C sambamba na Nigeria, Uganda na Tunisia ambao mechi zao zinapigwa kesho Jumanne, Tanzania ikivaana na Nigeria wajkati majirani zao wa Uganda wataumana na Tunisia.
RAIS wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Dk Patrice Motsepe ametangaza ongezeko la 43% la fedha za zawadi kwa bingwa wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 iliyoanza jana huko Morocco hadi kufikia Dola 10 milioni (zaidi ya Sh 24 Bilioni).
Tangazo hilo lilitolewa jana Jumamosi baada ya kikao cha Kamati ya Utendaji ya CAF kilichofanyika mjini Rabat, Morocco ikiwa ni saa chache kabla ya kuanza kwa michuano hiyo ya 35.
Fedha hizo za zawadi kwa bingwa zinaonesha ongezeko la asilimia 43 ikilinganishwa na fainali zilizopit zilizofanyika mwaka 2023 huko Ivory Coast ambapo wenyeji walibeba ubingwa na kuzawadiwa Dola 7 milioni (zaidi ya Sh17 bilioni).
Washindi wa AFCON 2021 zilizofanyikia Cameroon alizoa Dola 5 milioni (zidi ya Sh 12 bilioni) na kwa kuongezeka hadi kufikia Dola 10 milioni kwa fainali hizo za Morocco, kiasi hicho kinaashiria ongezeko la asilimia 100 ndani ya kipindi cha miaka minne.
Kwa upande mwingine, washindi wa pili wa michuano hiyo ya Morocco inayoshirikisha imu za nchi 24 ikiwamo Tanzania inayoshiriki kwa mara ya nne baada ya 1980, 2019 na 2023 atazawadiwa Dola 4 milioni( zaidi ya Sh 9 bilioni), huku timu mbili zitakazofika nusu fainali kila moja ikipata Dola 2.5 milioni (zaidi ya Sh6 bilioni).
Tanzania katika michuano hiyo imepangwa Kundi C sambamba na Nigeria, Uganda na Tunisia ambao mechi zao zinapigwa kesho Jumanne, Tanzania ikivaana na Nigeria wajkati majirani zao wa Uganda wataumana na Tunisia.