Benjamin Sesko apinga kuitwa ‘Super Sub’ ataka nafasi zaidi
Muktasari:
- Hilo linakuja wakati mteja wake akiendelea kufanya vyema kila anapoingia uwanjani kutokea benchi na kwenda kufunga mabao, lakini hajapewa nafasi zaidi ya kuanza kwenye kikosi cha kwanza cha Mashetani Wekundu.
MANCHESTER, ENGLAND: WAKALA wa mshambuliaji wa Manchester United, Benjamin Sesko, ameonyesha kutoridhishwa na nafasi yake chini ya kocha Michael Carrick, akipinga nyota huyo mwenye thamani ya Pauni 74 milioni kupewa jina la ‘super sub’
Hilo linakuja wakati mteja wake akiendelea kufanya vyema kila anapoingia uwanjani kutokea benchi na kwenda kufunga mabao, lakini hajapewa nafasi zaidi ya kuanza kwenye kikosi cha kwanza cha Mashetani Wekundu.
Sesko amefunga mabao tisa katika msimu wake wa kwanza kwenye Ligi Kuu England baada ya kuhamia kwa ada kubwa kutoka RB Leipzig majira ya kiangazi na kati ya mabao hayo, saba ameyafunga kuanzia mwanzo wa mwaka huu, huku Mslovenia huyo akionyesha kiwango bora tangu kuondoka kwa kocha Ruben Amorim mwezi Januari.
Mechi za Sesko katika Ligi Kuu England zimegawanyika sawa, akiwa ameanza michezo 13 na pia kuingia kama mchezaji wa akiba mara 13.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22 ameonekana kuwa muhimu anapoingia kutokea benchi chini ya Michael Carrick, akifunga mabao manne muhimu yaliyoisaidia timu hiyo katika harakati zake za kutaka kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Amefunga mabao ya ushindi dhidi ya Fulham na Everton, bao la kusawazisha dakika za mwisho dhidi ya West Ham United pamoja na bao la tatu lililothibitisha ushindi dhidi ya Aston Villa – yote baada ya kuingia kama mchezaji wa akiba.
Ufanisi huo ndio uliomfanya apewe jina la “super sub”, lakini wakala wake, Elvis Basanovic hapendi kabisa jina hilo.
“Kama utaniuliza kuhusu jina hilo, silipendi. Napendelea zaidi ‘super striker’. Nafikiri Benjamin ni mshambuliaji wa kiwango cha juu,” alisema na kuongeza:
“Ameanza michezo 13 mwaka huu na pia ameingia kama akiba mara 13. Amefunga nusu ya mabao yake akiwa ameanza na nusu akiwa ametokea benchi. Tunaona wazi kuwa yeye ni mshambuliaji thabiti na anastahili kuitwa ‘super striker’.”
Kumekuwa na wito wa Sesko kupewa nafasi zaidi ya kuanza kikosini kutokana na kiwango chake cha hivi karibuni, huku akianza mechi mbili tu chini ya Carrick. Alifunga bao alipokuwa kwenye kikosi cha kwanza katika ushindi wa 2-1 dhidi ya Crystal Palace Machi 1, lakini hakufunga katika kipigo cha 2-1 dhidi ya Newcastle siku tatu baadaye.
Mwezi Februari, Sesko alisisitiza kuwa yupo tayari kuisaidia timu bila kujali nafasi anayopata.
“Ninaendelea kuzoea ligi hatua kwa hatua. Sifikirii sana kuhusu lazima nianze. Kwangu, ni kocha ndiye anaamua. Nikipewa dakika tano tu nitazitumia vizuri. Kitu muhimu ni kufurahia na kutoa mchango kwa timu,” alisema.
Wakati huohuo, Manchester United ilitangaza Jumatatu, wiki hii kuwa Sesko amekuwa akicheza akiwa na majeraha madogo aliyoyapata hivi karibuni, na ameondolewa katika kikosi cha Slovenia ili kuhakikisha anapona kikamilifu.
Kikosi cha Carrick kimeingia katika mapumziko ya kimataifa kikiwa nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu England tofauti ya pointi sita dhidi ya Liverpool walio nafasi ya tano katika mbio za kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya.