Bellingham: Tuna bahati kufungwa bao 3 tu, zingekuwa nyingi

Muktasari:
- Real Madrid imekuwa na msimu mbaya ikiruhusu mabao mengi na katika mechi hiyo ya jana iliyofungwa 3-0, kipa wao Thibaut Courtois aliokoa hatari nyingi.
KIUNGO nyota wa Real Madrid, Jude Bellingham amesema timu yake ilikuwa na bahati sana kufungwa mabao matatu tu katika mechi yao ya mkondo wa kwanza wa hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwenye Uwanja wa Emirates jana usiku.
"Arsenal wangeweza kufunga mabao mengi zaidi, tulikuwa na bahati kufungwa bao 3 tu," amesema Jude.
"Kusema kweli, hatuna visingizio... tunapaswa kujiangalia sisi wenyewe. Ni jambo ambalo limetutokea msimu wote, lakini dhidi ya Arsenal limetokea kwa kiwango kikubwa zaidi.”
“Tutalazimika kulikabili hili na tutahitaji kitu cha kipekee ili kubadilisha hali hii. Kama kuna sehemu ambapo mabadiliko yanaweza kutokea, ni nyumbani kwetu, Bernabeu.”
Real Madrid imekuwa na msimu mbaya ikiruhusu mabao mengi na katika mechi hiyo ya jana iliyofungwa 3-0, kipa wao Thibaut Courtois aliokoa hatari nyingi.
Declan Rice aliifungia Arsema mabao mawili kwa frii-kiki na kuandika historia ya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga mabao mawili ya frii-kiki katika mechi moja hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Pia yalikuwa ni mabao ya kwanza kwa Rice kuwahi kufunga kwa frii-kiki katika maisha yake ya soka kwani hakuwahi kufunga bao hata moja la aina hiyo katika mechi 338.
Bao jingine la Arsenal lilifungwa na Mikel Merino. Timu hizo zitarudiana Jumatano Aprili 16, 2025 kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu.