Bayern yaweka mkono kwa Bruno Fernandes
Muktasari:
- Fernandes, ambaye ni mhimili muhimu wa kikosi cha Man United, bado ana mkataba wa kuwatumikia mashetani wekundu hadi mwaka 2027, lakini wababe hao wa Bundesliga wanamwona kama chaguo sahihi la kuimarisha safu yao ya kiungo.
BAYERN Munich ipo tayari kuwasilisha ofa ya takribani Euro 50 milioni kwenda Manchester United ili kumsajili kiungo na nahodha wa klabu hiyo, Bruno Fernandes, 31.
Fernandes, ambaye ni mhimili muhimu wa kikosi cha Man United, bado ana mkataba wa kuwatumikia mashetani wekundu hadi mwaka 2027, lakini wababe hao wa Bundesliga wanamwona kama chaguo sahihi la kuimarisha safu yao ya kiungo.
Man United bado haijaweka wazi msimamo wake kuhusu kumuuza au laa, lakini mara kadhaa imekuwa ikiripotiwa kuwa tayari kufanya hivyo ila kikwazo huwa kwa Bruno mwenyewe ambaye amekataa ofa takribani tatu kutoka Saudi Arabia.
Hivi karibuni staa huyo aliweka wazi kwamba Man United ilikubali kuchukua takribani Pauni 90 milioni kutoka kwa Al-Hilal ya Saudia katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi, lakini yeye alikataa kwenda. Msimu huu Bruno amecheza mechi 17 za michuano yote, amefunga mabao 5 na asisti saba.
Andre ter Stegen
ASTON Villa inaendelea kufuatilia kwa karibu maendeleo ya kipa wa Barcelona na timu ya taifa ya Ujerumani, Marc Andre ter Stegen, 33. ambaye anaripotiwa kutaka kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara ili kujiweka katika hali nzuri aweze kuitwa katika kikosi cha Ujerumani kitakachoenda kwenye Kombe la Dunia lijalo.
Kipa huyu mkongwe kwa sasa haonekani kuwa kipaumbele cha kocha Hansi Flick ambaye amekuwa akimchezesha Joan Garcia.
Nico Williams
WINGA wa Athletic Club na timu ya taifa ya Hispania, Nico Williams, 23, ameripotiwa kutaka kujiunga na Real Madrid, licha ya dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana kuwa karibu kujiunga na Barcelona. Williams ambaye pia huduma yake inahusudiwa sana na Liverpool, Arsenal na Chelsea, aliripotiwa ameshafikia hadi makubaliano binafsi na Barca kabla ya dili hilo kufeli katika dakika za mwisho alipochagua kusaini dili jipya Bilbao.
Gabriel Jesus
AC Milan inaangalia uwezekano wa kumsajili kwa mkopo mshambuliaji wa Arsenal na timu ya taifa ya Brazil, Gabriel Jesus, 28, katika dirisha lijalo la usajili.
Jesus amekuwa akipata wakati mgumu kupata nafasi ya kudumu katika kikosi cha kwanza cha Arsenal tangu alipopona majeraha ya muda mrefu, hali inayodaiwa kumlazimisha kufikiria kuondoka kwenda kutafuta changamoto mpya.
Ayyoub Bouaddi
ARSENAL imeanza mawasiliano na wawakilishi wa kiungo wa Lille, Ayyoub Bouaddi, 18, kuhusu uwezekano wa kumsajili katika dirisha la usajili la Januari kwa ada ya Euro 45 milioni.
Bouaddi, ambaye ni miongoni mwa vipaji vinavyochipukia kwa kasi barani Ulaya, kwa kipindi kirefu pia amekuwa akifuatiliwa kwa karibu na Manchester City, Manchester United na Liverpool, ambao maskauti wao wanamtazama.
Filip Jorgensen
KIPA wa Chelsea na timu ya taifa ya Denmark, Filip Jorgensen, 23, anataka kuondoka klabuni hapo baada ya kuchoshwa na nafasi yake ya kuwa chaguo la pili.
Jorgensen ana mkataba na Chelsea unaomalizika mwaka 2031, hivyo klabu itakayomhitaji itatakiwa kutoa ofa nzuri ili kumnunua au inaweza kumwomba kwa mkopo.
Staa huyu anataka kuondoka ili kucheza na kujiwekea nafasi kubwa ya kuitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Denmark ambacho bado kinapambana kufuzu kucheza Kombe la Dunia mwakani.
Nicolas Jackson
CHELSEA ipo tayari kumuuza mshambuliaji wake raia wa Senegal, Nicolas Jackson, 24, kwenda timu nyingine katika dirisha lijalo la usajili baada ya kuona Bayern Munich ambayo fundi huyo anacheza kwa mkopo kwa sasa kutokuwa na mpango wa kumsainisha mkataba wa moja kwa moja. Jackson, haonekani kuendelea kubaki katika klabu hiyo ya Ujerumani.
Semenyo
WINGA wa timu ya taifa ya Ghana, Antoine Semenyo, 25, ameipa kipaumbele Liverpool kama timu anayohitaji kujiunga nayo ikiwa ataondoka Bournemouth katika dirisha lijalo la usajili la Januari.
Semenyo
Semenyo anaripotiwa kuvutiwa zaidi na mradi wa Liverpool kuliko Manchester City na Manchester United, ambazo pia zimeonyesha nia ya kuitaka huduma yake.
Bournemouth inatajwa kuwa tayari kumuuza mchezaji huyo ikiwa itapokea ofa nono.