Bayern hawamtaki Haaland

Monday August 02 2021
bayern pic

MUNICH, UJERUMANI. RAIS wa Bayern Munich, Herbert Hainer amefunguka na kusema kwamba hawataingia kwenye vita ya kufukuzia huduma ya straika Erling Haaland na kusisitiza kwamba supastaa wao Robert Lewandowski atabaki kwenye kikosi hicho hadi mwisho wa mkataba wake.

Jambo hilo linaipa Chelsea matumaini makubwa juu ya kunasa saini ya Haaland, ambaye imemwekwa kwenye rada zake, akiwa mchezaji namba moja katika wanaowasaka kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi. Staa mwingine waliyekuwa wakimsaka ni Lewandowski, ambaye kwa mujibu wa Herbert Hainer, mchezaji huyo atabaki kwenye kikosi cha Bayern Munich hadi Juni 2023.

Haine alisema: “Robert Levandowski ataendelea kuichezea Bayern hadi Juni 2023. Ana mkataba wa kuendelea kubaki mahali hapa. Hatuhitaji straika mpya.”

Jambo hilo linakuja baada ya kuwapo na ripoti kwamba Bayern ilikuwa na uhakika mkubwa wa kumnasa Haaland mwakani wakati mchezaji huyo atakapokuwa anapatikana kwa Pauni 65 milioni kutokana na kipengele kilichowekwa kwenye mkataba wake.

Lakini, kwa mujibu wa maelezo ya Hainer, anaamini Bayern haitahangaika kutafuta mrithi Lewandowski walau hadi hapo itakapofika mwaka 2023.

Straika huyo wa zamani wa Borussia Dortmund, Lewandowski, 32, ataingia msimu wake wa nane kwenye kikosi hicho cha Bayern na haonekani ikuchuja.

Advertisement
Advertisement