Barcelona yalia refa kaiua

Muktasari:
- Barca ilionekana kama ingetinga hatua ya fainali baada ya bao la Raphinha katika dakika ya 87 kuwafanya kuongoza 3-2, lakini Inter ilisawazisha dakika za majeruhi na kulazimisha mechi hiyo kuingia kwenye dakika 30 za ziada.
MILAN, ITALIA: BARCELONA imemshushia lawama mwamuzi Szymon Marciniak baada ya kuchapwa kwenye mechi ya marudiano ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na kutupwa nje ya michuano hiyo na Inter Milan katika mechi ya funga nikufunge usiku wa Jumanne huko San Siro.
Barca ilionekana kama ingetinga hatua ya fainali baada ya bao la Raphinha katika dakika ya 87 kuwafanya kuongoza 3-2, lakini Inter ilisawazisha dakika za majeruhi na kulazimisha mechi hiyo kuingia kwenye dakika 30 za ziada.
Beki veterani Francesco Acerbi aliingia kati kucheza nafasi ya mshambuliaji wa kati na kumalizia krosi ya Denzel Dumfries katika dakika ya 93 kufanya ubao wa matokeo usomeke 3-3 huku matokeo ya jumla yakiwa 6-6.
Davide Frattesi baadaye aligeuka kuwa nyota wa mchezo, alipofunga bao maridadi kabisa, huku kipa wa Inter Milan, Yann Sommer akifanya kazi ya ziada kuokoa hatari nyingi kulinda ushindi huo.
Ilikuwa mechi ya funga nikufunge huku mwamuzi Marciniak alikuwa na kazi kubwa ya kufanya. Aliipa Inter penalti baada ya Pau Cubarsi kumchezea rafu Lautaro Martinez baada ya VAR kumwita mwamuzi akatazame picha za marudio kwenye skrini iliyokuwa pembeni ya uwanja kabla ya VAR kutumika pia kubadili mkwaju wa penalti wa Barcelona kuwa friikiki baada ya Henrikh Mkhitaryan kumchezea madhambi Lamine Yamal nje ya boksi.
Barca ilikasirishwa na bao la kusawazisha la Inter, ikiamini Dumfries alimfanyia madhambi Gerard Martin kabla ya kufungwa bao hilo. Kocha Hansi Flick na mchezaji wa akiba Pau Victor walionyeshwa kadi za njano na mwamuzi Marciniak baada ya kulalamikia bao hilo.
“Hii si mara ya kwanza kututokea sisi kwa mwamuzi huyu na nadhani UEFA inapaswa kulitazama. Kuna vitu ni vigumu kuvielezea,” alisema kiungo wa Barca, Pedri alipozungumza na El Partidazo de Cope.
“Kuna matukio mengi sana. Kila tukio la 50/50 lilikwenda upande wetu na ile penalti ya Lamine, ambayo ilibadilishwa na kuwa friikiki, hakumwonyesha kadi ya njano Mkhitaryan, ambayo ingekuwa ya pili.”
Eric Garcia naye alimshambulia refa Marciniak alipozungumza na Movistar Plus: “Soka limekuwa likitufanyia isivyo. Nimekuja kwenye uwanja wa Inter Milan mara tatu na mara zote vitu vilivyokuwa nje ya uwezo wetu ni lazima vitokee. Sote tunafahamu kilichotutokea kwa mwamuzi huyu tulipokuja hapa mara ya mwisho. Lakini, haina kujitetea, wamefunga mabao zaidi ya sita dhidi yetu.”
Kocha Flick naye alisema: “Sitaki kuzungumza sana kuhusu mwamuzi, lakini kila matukio ya 50-50 yaliwafaidisha Inter. Nimehuzunika, lakini sikuhuzunishwa na timu yangu. Walijaribu kila kitu. Ndiyo hivyo, tumetoka, lakini mwakani tutajaribu tena kuwafurahisha mashabiki wetu. Imenihuzunisha kwa sababu timu yangu imefanya kazi nzuri. Sipendi kuzungumza kuhusu mwamuzi, nilishamwambia nilichokuwa nafikiri, lakini siwezi kukisema hapa, nilichomwambia.”