Man United, Athletic Bilbao kitawaka Europa League

Muktasari:
- Huko Manchester, uwanjani Old Trafford, Manchester United itakuwa nyumbani kukipiga na Athletic Bilbao katika mechi ya marudiano baada ya kushinda 3-0 ugenini Hispania, Alhamisi iliyopita.
MANCHESTER, ENGLAND: MAMBO ni moto. Kivumbi cha mechi za nusu fainali kwenye michuano ya Ulaya kinahamia kwenye mikikimikiki ya Europa League, ambapo vigogo wanne watapigana vikumbo kutafuta nafasi ya kucheza fainali itakayopigwa mjini Bilbao, Hispania, Mei 21.
Huko Manchester, uwanjani Old Trafford, Manchester United itakuwa nyumbani kukipiga na Athletic Bilbao katika mechi ya marudiano baada ya kushinda 3-0 ugenini Hispania, Alhamisi iliyopita.
Kipute kingine cha marudiano kitakuwa huko Norway, ambapo Bodoe/Glimt itakuwa na kazi ya kujaribu kupindua meza mbele ya Tottenham Hotspur baada ya kuchapwa mabao 3-1 katika mchezo wa kwanza wa nusu fainali uliofanyika London, England.
Spurs itakuwa ugenini kucheza na Bodoe/Glimt, ambayo moja ya sifa kubwa ya timu hiyo wachezaji hawakati tamaa, wanakomaa mwanzo mwisho. Bao lao la ugenini linawapa matumaini ya kwamba wakifunga mara mbili bila ya majibu ubao utasomeka 3-3 na hapo watakuwa kwenye mchakato muhimu wa kutafuta ushindi.
Na kuhusu bao hilo la ugenini limewapa matumaini ya kufanya kweli Aspmyra na taarifa yao ilisomeka hivi: “Lilikuwa bao muhimu sana. Limetupa matumaini kwa mechi ya nyumbani, kwa sababu 3-0 tungekuwa tushatoka, pengo ni kubwa sana. Kama tulijifunga mengi kwenye ile mechi, tutakwenda kufanya vizuri kwenye mechi ijayo.”
Kwenye mikikimikiki hiyo ya Europa League msimu huu, Bodoe/Glimt imefanya mambo ya kushangaza, ikizichapa Maccabi Tel-Aviv, Twente, Olympiacos na Lazio nyumbani kwa tofauti ya mabao mawili, huku pia katika mchezo huo wa usiku wa Alhamisi itawakaribisha kikosini nyota wao watatu muhimu, Patrick Berg, Hakon Evjen na Andreas Helmersen, ambao wote hawakucheza mechi ya kwanza.
Spurs inahitaji kushinda ubingwa wa Europa League ili kukamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao baada ya mambo kubwa magumu kwenye Ligi Kuu England, ikishika nafasi ya 16 katika msimamo. Hicho, kipute hicho cha usiku, shughuli ipo.
Huko Old Trafford, mashabiki wa Man United wanaamini timu yao itaweza kulinda uongozi wao wa mabao 3-0 iliyoupata ugenini San Mames ili kuwasukuma nje Bilbao na kutinga fainali ya michuano hiyo ya Europa League.
Man United yenyewe pia inahitaji ubingwa wa Europa League ili kukamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao baada ya hali kuwa ngumu kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, ambapo inashika nafasi ya 15.
Rekodi zinaonyesha kwamba ni mara moja tu timu iliyokuwa inaongoza mabao matatu kwenye mechi ya kwanza kwenye michuano ya Europa League ilishindwa kusonga mbele, wakati Valencia ilipindua meza dhidi ya FC Basel na kushinda 5-3 kwenye matokeo ya jumla katika robo fainali ya msimu wa 2013/14 baada ya kupoteza 3-0 ugenini huko Uswisi.
Kwenye michuano yote ya Ulaya msimu huu, Man United ndiyo timu pekee ambayo bado haijapoteza, hivyo ushindi wa mabao 3-0 ugenini umewaweka kwenye nafasi nzuri katika mechi hiyo ya marudiano, ambapo kocha Ruben Amorim anaamini vijana wake watafanya kweli.
Kinachoipa nguvu Bilbao ni kwamba iliwahi kushinda Old Trafford, wakati ilipoichapa Man United mabao 3-2 katika mchezo wa kwanza wa hatua ya 16 bora kwenye msimu wa 2011/12. Lakini, mtihani unaoikabili safari hii, itahitaji kufunga mara tatu bila ya majibu huku ikiamini kwamba mastaa wake kama Inaki na Nico Williams watafanya hilo liwezekane.
Kumbukumbu zinaonyesha kwamba Man United imepoteza mara moja tu kati ya mechi 10 za mwisho ilizocheza dhidi ya timu za Hispania, imeshinda sita na sare nne. Fainali ya mwaka huu ya Europa League itapigwa kwenye Uwanja wa San Mames, Bilbao, Hispania.