Osimhen sasa arejea kwenye rada za Atletico Madrid
Muktasari:
- Victor Osimhen ni mshambuliaji wa kiwango cha juu aliyethibitisha uwezo wake. Ana kasi katika nafasi wazi, ni mkali ndani ya eneo la hatari na ana uwezo wa kufunga mabao kwa mwendelezo katika misimu ya hivi karibuni.
VICTOR Osimhen amerejea kwenye rada za Atletico de Madrid kama moja ya machaguo ya kuimarisha safu ya ushambuliaji.
Mshambuliaji huyo wa Nigeria, aliye katika kilele cha kiwango chake cha soka, anaendana na wasifu wa straika mwenye nguvu na ushawishi ambao klabu hiyo inautafuta ili kuongeza ubora wa kikosi.
Hata hivyo, dili hilo si rahisi. Kikwazo kikubwa si cha kiufundi, bali ni cha kifedha.
Victor Osimhen ni mshambuliaji wa kiwango cha juu aliyethibitisha uwezo wake. Ana kasi katika nafasi wazi, ni mkali ndani ya eneo la hatari na ana uwezo wa kufunga mabao kwa mwendelezo katika misimu ya hivi karibuni. Anaonekana kuwa chaguo linalofaa kwa mfumo wa ushindani wa Atltico Madrid.
Ndani ya klabu wanaamini kuwa nguvu zake, presha yake ya juu na uwepo wake wa kimwili vitafaa kikamilifu katika mbinu za kocha Diego Simeone. Aidha, mchezaji huyo yuko tayari kusikiliza ofa.
Mateus Mane
WOLVES imekata tamaa na inaona ina asilimia ndogo za kumbakisha mshambuliaji wake kinda Mateus Mane, 18, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Mane, ambaye pia ni mchezaji wa timu za vijana za England, anawindwa na vigogo wa Ligi Kuu England ambao ni pamoja na Liverpool, Manchester United na Arsenal. Inaelezwa kuwa Wolves inafahamu itakuwa vigumu kumbakisha staa huyo kutokana na ushindani mkubwa wa timu zinazomhitaji na ofa nono zinazotarajiwa kuwasilishwa.
Liam Delap
EVERTON imemweka mshambuliaji wa Chelsea, Liam Delap, 23, katika orodha ya mastaa ambao inataka kuwasajili katika dirisha lijalo la usajili wa majira ya kiangazi. Delap alijiunga na Chelsea msimu uliopita akitokea Ipswich Town, lakini bado hajapata nafasi ya kudumu katika kikosi cha kwanza hali iliyochochea tetesi za kuondoka kwake. Everton inaamini uwezo wa Delap ni mkubwa na inahitaji kumpata walau kwa mkopo ikiwa itashindikana kumnunua jumla.
Harvey Elliott
ASTON Villa bado haijatoa Pauni 35 milioni kumsainisha mkataba wa moja kwa moja kiungo wa Liverpool, Harvey Elliott, 22, ambaye anacheza kwa mkopo katika kikosi chao akitokea Liverpool.
Villa haijafanya hivyo, kwa sababu kifungu kinachowataka kumsainisha mkataba wa moja kwa moja kitakuwa halali mara tu, atapocheza zaidi ya mechi 20 za Ligi Kuu England msimu huu.
Harry Kane
MGOMBEA wa nafasi ya urais wa Barcelona, Xavier Vilajoana ametoa ahadi ya kumsajili mshambuliaji wa Bayern Munich na timu ya taifa ya England Harry Kane, 32, ikiwa atachaguliwa kuwa rais wa timu hiyo katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao. Vilajoana amemjumuisha Kane katika kampeni zake akiamini huyo ndio atakuwa mbadala sahihi wa Robert Lewandowski ambaye kuna asilimia kubwa akaondoka Barca mwisho wa msimu huu.
Lucas Bergvall
TOTTENHAM Hotspur imesisitiza kuwa haina mpango wa kumuuza kiungo wake wa kimataifa wa Sweden, Lucas Bergvall, 20, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi licha ya kupokea ofa kutoka kwa Aston Villa na Chelsea mwezi uliopita.
Bergvall anaonekana kuwa sehemu muhimu ya mipango ya muda mrefu ya Spurs, baada ya kuonyesha kiwango bora tangu ajiunge na klabu hiyo.
Nico Paz
REAL Madrid itamrudisha kiungo wa kimataifa wa Argentina Nico Paz, 21, iliyemuuza kwenda Como ya Italia miaka miwili iliyopita. Paz, ameivutia sana Madrid kutokana na kufanya vizuri katika Serie A katika misimu miwili aliyohudumu hadi sasa.
Uongozi wa Madrid unamwona kama sehemu ya mkakati wao wa kuendelea kuimarisha kikosi kupitia wachezaji vijana.
Jarell Quansah
LIVERPOOL imeanza harakati tena za kumsajili beki wa kati raia wa England, Jarell Quansah, 23, anayeitumikia Bayer Leverkusen ya Ujerumani. Quansah, aliyesajiliwa na Leverkusen akitokea Liverpool, amekuwa akionyesha kiwango bora ambacho kimezivutia timu nyingi barani Ulaya. Taarifa zinaeleza kuwa Liverpool iliweka kipengele cha kumrejesha mchezaji huyo (buy-back clause), kwa kiasi maalum ikiwa watamhitaji.