Anthony Gordon aangaliwa kuwa mbadala wa Salah
Muktasari:
- Vyanzo vinaeleza kuwa Liverpool tayari imeanza kutafuta mbadala wa Salah na wanaamini Gordon ana kasi, nguvu na uwezo wa kucheza katika mifumo tofauti ya ushambuliaji.
LIVERPOOL inaandaa ofa ya Pauni 83 milioni kumsajili winga wa Newcastle United na timu ya taifa ya England, Anthony Gordon, 24, ikiwa mshambuliaji wao wa kimataifa wa Misri Mohamed Salah, 33, ataondoka katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Vyanzo vinaeleza kuwa Liverpool tayari imeanza kutafuta mbadala wa Salah na wanaamini Gordon ana kasi, nguvu na uwezo wa kucheza katika mifumo tofauti ya ushambuliaji.
Hata hivyo, Newcastle hawako tayari kumwachia kirahisi staa huyo ambaye kwa sasa ni miongoni mwa mastaa wao tegemeo katika kikosi cha kwanza.
Gordon ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2030, tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 37 za michuano yote na kufunga mabao 14.
Taarifa zinadai Salah ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu ujao kuna asilimia kubwa akatimkia Al Ittihad ya Saudi Arabia ambayo inatafuta straika baada ya Karim Benzema kuondoka.
Uwezekano wa dili hili kukamilika mbali ya kuwa mikononi mwa Newcastle yenyewe kwa asilimia kubwa, pia upo kwa Gordon mwenyewe ambaye haonekani kuwa na uhitaji sana wa kuondoka kwani alikataa ofa kadhaa kutoka kwa timu zilizomhitaji.
Darwin Nunez
TOTTENHAM na Newcastle United zimeanza rasmi kuiwania saini ya mshambuliaji wa Al-Hilal, Darwin Nunez, 26, kuelekea dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Nunez, ambaye aliwahi kung'ara akiwa na Liverpool, bado anatajwa kuwa kwenye rada za klabu kadhaa za EPL zinazotaka kuboresha kikosi chao.
Inaelezwa kuwa Spurs inataka mshambuliaji mwenye nguvu na kasi baada ya kufanya vibaya kwa msimu huu.
Mkataba wa sasa wa Nunez unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.
Pavel Sulc
TOTTENHAM na Aston Villa ni kati ya klabu zinazomfuatilia kwa karibu kiungo wa Olympique Lyon, Pavel Sulc, 25, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Sulc amekuwa akionyesha kiwango bora katika Ligi Kuu Ufaransa ambacho kimewavutia mabosi wa timu nyingi Ulaya.
Hata hivyo, Lyon hawana haraka ya kumwachia, lakini ofa nono inaweza kuwafanya kufikiria kumuuza staa huyo raia wa Jamhuri ya Czech.
Joe Gomez
BEKI wa Liverpool, Joe Gomez, 28, anaonekana kuwa kwenye mpango wa kuondoka katika kikosi hicho mwishoni mwa msimu huu, huku AC Milan na Bayern Munich zikiripotiwa kutaka kumsajili.
Gomeznamekuwa akikabiliwa na ushindani mkubwa wa namba katika kikosi cha kwanza cha Liveprool hali inayosababisha asipate nafasi kubwa ya kucheza katika kikosi cha kwanza.
Liverpool haijafunga milango ya kumwachia staa huyu ikiwa ofa nzuri itawasilishwa mezani kwao. Mkataba wa Gomez na majogoo hawa unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.
Marcos Senesi
ROMA na Juventus zipo katika vita ya kutaka kumsajili beki wa Bournemouth, Marcos Senesi, 28, mwisho wa msimu huu.
Senesi amekuwa mhimili muhimu katika safu ya ulinzi ya Bournemouth, lakini hata yeye mwenyewe anaonekana kupendelea kwenda Italia ikiwa moja kati ya timu hizo zitafikia makubaliano na Bournemouth.
Inaelezwa kuwa mchezaji huyo yuko tayari kurejea Italia ambako aliwahi kucheza awali na Bournemouth ipo tayari kusikiliza ofa kutoka timu zinazomhitaji.
Nico Schlotterbeck
REAL Madrid ipo katika nafasi nzuri kushinda vita ya kumsajili beki wa Borussia Dortmund na timu ya taifa ya Ujerumani, Nico Schlotterbeck, 26, ambaye pia anawindwa na Barcelona, inayomhitaji sana.
Mazungumzo baina ya mabosi wa Dortmund na wawakilishi wa staa huyu yanaendelea, lakini hadi sasa hakuna makubaliano yaliyofikiwa. Mkataba wa Schlotterbeck unatarajiwa kumalizika mwaka 2027. Tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 26 za michuano yote.
Hugo Bueno
NEWCASTLE United ina nia ya kumsajili beki wa Wolves, Hugo Bueno mwenye umri wa miaka, 23, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Bueno, ambaye ni raia wa Hispania, amekuwa akionyesha kiwango bora akiwa na Wolves, jambo lililovutia macho ya benchi la ufundi la Newcastle wanaotaka kuboresha kikosi chao.
Inaelezwa kuwa Newcastle wako tayari kuanza mazungumzo ikiwa Wolves watakuwa tayari kumuuza, lakini hadi sasa hakuna majadiliano yoyote yaliyofanywa.
Liam Delap
EVERTON ipo tayari kumpa ofa ya Pauni 30 milioni kumsajili mshambuliaji wa Chelsea, Liam Delap, 23, katika dirisha lijalo la usajili.
Delap hajapata nafasi ya kudumu Stamford Bridge tangu ajiunge na Chelsea, jambo lililochochea hali ya kutaka kuondoka kwake.
Everton inaamini Delap anaweza kuwa suluhisho la matatizo yao ya ufungaji mabao na wako tayari kufanya mazungumzo ya haraka, ingawa uamuzi wa mwisho utategemea msimamo wa Chelsea.