Barcelona kusafiri umbali wa maili 10,000
Muktasari:
- Miamba hiyo ya LaLiga itasafiri kwenda Miami, Marekani kwenda kukabiliana na Villarreal katika mchezo wa ligi utakaofanyika Desemba 21.
BARCELONA, HISPANIA: BARCELONA inakabiliwa na kasheshe la kusafiri umbali wa karibu maili 10,000 siku chache kabla ya Krismasi kwenda kucheza mechi ya La Liga nje ya Hispania.
Miamba hiyo ya LaLiga itasafiri kwenda Miami, Marekani kwenda kukabiliana na Villarreal katika mchezo wa ligi utakaofanyika Desemba 21.
Na sasa Marcus Rashford na wachezaji wenzake watakuwa na kazi ya kusafiri karibu maili 5,000kwa ndege kwenda kwenye mechi hiyo na maili nyingine 5,000 kurudi Hispania.
Umbali wa moja kwa moja kutoka Barcelona, Hispania hadi Miami, Florida ni maili 4,700 kuvuka Bahari ya Atlantic.
Mechi hiyo kati ya Barcelona na Villarreal itapigwa uwanjani Hard Rock huko Marekani, itakuwa ya kwanza kwa mchezo wa La Liga kuchezwa kwenye ardhi ya nchi ya kigeni.
Mechi hiyo itachezwa wiki moja baada ya kikosi hicho cha kocha Hansi Flick kukabiliana na Osasuna kwenye mchakamchaka huo wa michuano ya La Liga.
Kitu kizuri kwa wachezaji ni kwamba baada ya mechi hiyo ya Marekani hawatakuwa na mchezo mwingine hadi Januari 4, ambapo wachezaji watatumia muda huo kujiweka fiti kwa uchovu wa safari ndevu. Na mchezo huo kwenye Mwaka Mpya 2026 utapigwa uwanjani RCDE, kukabiliana na Espanyol kwenye mikikimikiki ya LaLiga.
Rais wa Barcelona, Joan Laporta anaamini mechi hiyo ni kitu kizuri kwao kwa sababu itaruhusu klabu yake kuwa na muunganiko mzuri na mashabiki wao wa kimataifa.
Alisema: “Tunasubiri kwa hamu kuungana na mashabiki wetu wa kimataifa huko Marekani na hili ni jambo zuri kwa La Liga kufungua mipango mbadala kwenye ishu ya masoko.”
Rais wa LaLiga, Javier Tebas aliielezea mechi hiyo kuwa ni hatua nzuri kihistoria ambapo itakwenda kulinufaisha soka la Hispania.