Barcelona ina jambo na Haaland
Muktasari:
- Vigogo hao wa LaLiga wamekuwa wakikumbwa na matatizo ya kifedha yaliyowalazimisha kutofanya usajili wa kutosha katika madirisha ya usajili ya hivi karibuni.
BARCELONA, HISPANIA: BAECELONA imesisitiza kwamba ina fedha za kutosha kuwasilisha ofa kwenda Manchester City kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji wa klabu hiyo na timu ya taifa ya Norway, Erling Haaland, endapo atakuwa tayari kujiunga nao.
Vigogo hao wa LaLiga wamekuwa wakikumbwa na matatizo ya kifedha yaliyowalazimisha kutofanya usajili wa kutosha katika madirisha ya usajili ya hivi karibuni.
Hata hivyo, mmoja wa wajumbe wakuu wa bodi yao, Joan Soler, anadai kuwa watawasilisha ofa ya kumsajili Haaland iwapo Man City itakuwa tayari kumuuza.
Soler alisema: "Ndiyo, tunaweza kusajili wachezaji kama Julian Alvarez au Haaland.
"Usajili wa aina hii hujilipa wenyewe ndani ya miaka mitano na hali ya kifedha ya Barca iko tayari kwa jambo kama hili."
Hata hivyo, Haaland bado ana mkataba wa muda mrefu na Man City na atahitajika kukubali mshahara mdogo tofauti na ule ambao anaupata kwa sasa.
Soler aliongeza: "Mwisho wa yote, Barca lazima iwe makini sana na usajili inaoufanya kwa kuzingatia mzigo wa mishahara. Tumejiwekea kikomo na hatutaki kuvuka. Lazima tusajili wachezaji kwa bei za kawaida."
Haaland alijiunga na Man City akitokea Borussia Dortmund mwaka 2022 na akachukua tuzo ya mfungaji bora wa Ligi Kuu England katika misimu yake miwili ya kwanza mfululizo akiwa katika viunga hivyo vya Etihad.
Hata hivyo, Barcelona huenda ikamgeukia staa mwingine wa Man City, Omar Marmoush, iwapo itaona Haaland ni ngumu kumsajili.
Mabingwa watetezi wa LaLiga wamekuwa wakimfuatilia Marmoush tangu alipokuwa Eintracht Frankfurt na ilishindwa kumsajili kwa wakati huo kutokana na kiasi kikubwa cha pesa kilichohitajika.
Kumekuwa na tetesi kuwa Marmoush alikuwa tayari kuondoka City kabla ya dirisha la majira ya baridi kufungwa, kutokana na kushindwa kupata nafasi kubwa ya kucheza katika kikosi cha kwanza.