Barca yabadilisha msimamo kwa De Jong

Muktasari:
- Licha ya kuanza mazungumzo hayo, ripoti zinadai Arsenal ni miongoni mwa timu zinazohitaji saini ya fundi huyu wa kimataifa wa Uholanzi ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwakani.
BARCELONA inafanya mazungumzo na wawakilishi wa kiungo wao Frenkie de Jong, 27, kwa ajili ya kumsainisha mkataba mpya utakaomwezesha kusalia katika timu hiyo kwa muda mrefu.
Licha ya kuanza mazungumzo hayo, ripoti zinadai Arsenal ni miongoni mwa timu zinazohitaji saini ya fundi huyu wa kimataifa wa Uholanzi ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwakani.
Awali Barca ilidaiwa kutaka kuachana na staa huyu na moja kati ya sababu kubwa ikiwa ni kutoonyesha kiwango cha kuridhisha hali iliyosababisha hata mashabiki kumzomea.
Tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 28 za michuano yote, amefunga mabao mawili na kutoa asisti moja.
Mbali ya Arsenal, mara kadhaa mashetani wekundu wa Jiji la Manchester, Man United nao walihusishwa na mpango wa kumsajili lakini ilishindikana.
Dean Huijsen
REAL Madrid, Bayern Munich, Chelsea na Tottenham zote zinapambana vita kali kwa ajili ya kumsajili beki wa Bournemouth raia wa Hispania, Dean Huijsen, 19, dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Kwa mujibu wa Daily Mail, Bournemouth inahitaji kiasi kisichopungua Pauni 50 milioni au zaidi ilj kumuuza. Msimu huu kwenye mechi za Ligi Kuu England amecheza jumla ya michezo 21 na kufunga mabao mawili huku akionyesha kiwango bora.
Mason Greenwood
Atletico Madrid inataka kutuma ofa inayofikia Pauni 50 milioni kwenda Marseille ili kumsajili mshambuliaji wa timu hiyo na Jamaica, Mason Greenwood, 23, dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Greenwood ambaye msimu uliopita alicheza kwa mkopo Getafe amekuwa na kiwango bora tangu kuanza kwa msimu huu chini ya Roberto de Zerbi. Greenwood amekuwa na msimu mzuri akiwa mmoja wa vinara wa kutupia akiwa na mabao 15.
Joshua Kimmich
LICHA ya ripoti za hivi karibuni kudai ana nafasi kubwa ya kuondoka dirisha lijalo la majira ya kiangazi, kiungo wa Bayern Munich, Joshua Kimmich anadaiwa kuwa na uwezekano mkubwa wa kuendelea kuitumikia timu hiyo kwa msimu ujao na huenda akasaini hadi mkataba mpya wa muda mrefu. Awali staa huyu aliripotiwa huenda akatua Arsenal au Paris St-Germain.
Jesus Rodriguez
BAADA ya kutuma wawakilishi wake kwenda Hispania kwa ajili ya kumtazama winga wa Real Betis na Hispania, Jesus Rodriguez, 19, inaelezwa Chelsea imevutiwa na kiwango chake na huenda ikatoa Pauni 42 milioni kama ada ya uhamisho ambayo ndio inahitaji ili kuuzwa. Mbali na Chelsea, Liverpool pia inahitaji saini ya staa huyu.
Ederson
MANCHESTER United ina matumaini makubwa ya kumsajili mshambuliaji wa RB Leipzig, Benjamin Sesko, 21, dirisha lijalo la majira ya kiangazi kwa kulipa Euro 80 milioni inayohitajika kwa mujibu wa mkataba wake. Sesko ambaye huduma yake pia inahitajika na Liverpool ni miongoni mwa mastaa wanaowindwa na timu mbalimbali barani Ulaya kutokana na kiwango alichoonyesha msimu uliopita.
Benjamin Sesko
MANCHESTER United na Liverpool zimeulizia uwezekano wa kuipata huduma ya kiungo wa Atalanta na timu ya taifa ya Brazil, Ederson, 25, ambaye awali alitajwa anaweza kutua Manchester City. Kwa mujibu wa ripoti, Atalanta inahitaji zaidi ya Pauni 50 milioni ili kumuuza mchezaji huyu kwa dirisha lijalo.
Harvey Elliott
LIVERPOOL ipo tayari kumtoa kwa mkopo kiungo wao raia wa England, Harvey Elliott, 21, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi ili ajiunge na timu itakayompa nafasi kubwa zaidi ya kucheza tofauti na ilivyo sasa. Elliott ambaye amefunga mara kadhaa alizoingia msimu huu akitokea benchi aliomba kutolewa kwa mkopo tangu dirisha lililopita lakini Liverpool ilikataa.