Barca bila ya Messi yagawa dozi

Muktasari:
Messi amevunjika mkono na atakuwa nje kwa muda wa zaidi wa wiki mbili jambo litakalomfanya akose mechi ya El Clasico itakayopigwa Jumamosi
Madrid, Hispania. Licha ya kutokuwa na mshambuliaji nyota Lionel Messi, Barcelona usiku wa kuamkia leo ilimpa raha nahodha wake baada ya kushinda mabao 2-0 dhidi ya Inter Milan.
Messi alikuwa jukwaani na mwanaye kwenye Uwanja wa Nou Camp, kutokana na jeraha la mkono aliloumia mwishoni mwa wiki.
Messi atakuwa nje ya uwanja wiki tatu, baada ya kuvunjika mkono wa kulia. Rafinha na Jordi Alba walifunga mabao hayo.
Kocha Ernesto Valverde amejiweka katika nafasi kwenye mbio za kuwania ubingwa wa Ulaya baada ya Barcelona kukwea kileleni ikiongoza Kundi B kwa pointi tisa baada ya kushinda mechi zote tatu.
Awali, mashabiki wa Barcelona walikuwa na hofu kama timu hiyo itashinda mchezo huo kutokana na kukosekana kwa Messi.
Barcelona ilicheza soka kwa kiwango bora na kuwabana wapinzani wao katika mchezo huo.
Inter Milan ilikuwa na nafasi ya kufunga, lakini mshambuliaji Ivan Perisic licha ya kumtoka beki Gerard Pique, alishindwa kuweka mpira wavuni.
Pia, Sergio Roberto na Mauro Icardi walishindwa kuisaidia Inter Milan kupata angalau bao katika mchezo huo licha ya kuonekana kuwa tishio katika safu ya ushambuliaji.
Barcelona nusura ifunge bao kupitia kwa mchezaji Clement Lenglet aliyepiga mpira wa kichwa kufuatia kona ya Philippe Coutinho lakini kipa Samir Handanovic aliokoa.
Katika mechi nyingine, PSG ililazimishwa sare ya mabao 2-2 na Napoli, Borussia Dortmund ilipata ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Atletico Madrid. Porto iliilaza Lokomotiv Moscow mabao 3-1.