Banchero alivyorudi kwa kishindo NBA
Muktasari:
- Banchero ambaye alikosekana uwanjani katika michezo 34 akiuguza majeraha ya misuli alishindwa jana kuinusuru Orlando Magic na kipigo, licha ya kufanya mambo makubwa kwenye mchezo huo.
FLORIDA, MAREKANI: KATIKA mchezo wake wa kwanza tangu Oktoba 30, mwaka jana alipokosekana kutokana na majeraha ya misuli, Paolo Banchero amerejea kwa kishindo katika Ligi ya Kikapu Marekani (NBA) akifunga alama 34 licha ya timu yake, Orlando Magic, kupoteza kwa pointi 109-106 dhidi ya Milwaukee Bucks.
Banchero ambaye alikosekana uwanjani katika michezo 34 akiuguza majeraha ya misuli alishindwa jana kuinusuru Orlando Magic na kipigo, licha ya kufanya mambo makubwa kwenye mchezo huo.
Mara baada ya mchezo huo Kocha wa Orlando, Jamahl Mosley alisema: “Sikuwa na matarajio kama haya, lakini ndivyo ilivyokuwa. Alikuwa akifanya kazi kwa bidii ili kurudi na kile alichofanya kilionyesha jitihada zake.
“(Banchero) alikuwa na ustahimilivu na alichukua mipira sahihi kwa wakati sahihi. Hii inadhihirisha jinsi anavyotaka kufikia malengo yake. Huyu ni mchezaji mwenye nyota kwa sababu ya uwezo wake.”
Banchero alifunga kwa asilimia 52 (11 kwa 21), akionyesha kuwa anarejea katika kiwango cha juu baada ya muda mrefu wa kuwa mbali na uwanja.
Nyota huyo anakiri kuwa kipindi cha majeraha kilimfanya kuwa na mashaka kutokana na maumivu, lakini sasa ana imani kubwa atafanya mambo mazito baada ya kurejea.
“Sio kwamba nilikuwa nahuzunika sana, lakini ni vigumu kukosa mechi na ukafurahi. Sijawahi kukosekana muda mrefu hivi tangu nilipoanza kucheza mpira wa kikapu. Nilikuwa tayari kwa msimu, lakini kuumia mapema ilifanya nijiulize ‘kwa nini?” anaeleza Banchero.
Ingawa alikosekana uwanjani, Banchero alikuwa sehemu muhimu ya timu akishiriki kila wakati kwenye vikao vya makocha na pia akiwa kwenye benchi kuwasaidia wachezaji wakiwa mchezoni.
“Nilijaribu kutafuta mambo chanya. Nilikuwa na nafasi ya kujifunza mpira kwa mtindo mwingine. Lakini sasa, nadhani nina ari zaidi. Inavyoonekana, baadhi ya vitu vilichukuliwa kwangu kwa muda, lakini sasa nipo tena uwanjani na najua kuwa lazima nirekebishe kilichokosekana,” alisema.
Wakati Banchero alipokuwa majeruhi, Orlando ilifanya vizuri zaidi kuliko ilivyotarajiwa ikishindwa katika michezo minne ya mwanzo, lakini ilishinda michezo 19 na baadaye kupoteza 11 katika kipindi kilichobaki cha majeraha yake.
Hata hivyo, baada ya kushindwa kwa pointi 109-106 dhidi ya Milwaukee Bucks jana, Orlando ilishuka nafasi kutoka ya nne hadi ya tano katika mashindano hayo Ukanda wa Mashariki.