Bafana Bafana katikati ya mtego AFCON 2025
Muktasari:
- Rekodi zinaonyesha katika michuano 11 iliyoyowahi kushiriki awali, Bafana Bafana imeshinda mechi tatu, ikapoteza nne na kutoka sare nne zikiwemo mbili dhidi ya Angola inayokutana nao leo Jumatatu.
TIMU ya taifa ya Afrika Kusini, Bafana Bafana leo Jumatatu inatarajiwa kushuka uwanjani kukata utepe wa merchi za Kundi B ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 dhidi ya Angola, ikiwa na mtihani wa kuepuka gundu mechi za ufunguzi katika fainali za michuano hiyo.
Rekodi zinaonyesha katika michuano 11 iliyoyowahi kushiriki awali, Bafana Bafana imeshinda mechi tatu, ikapoteza nne na kutoka sare nne zikiwemo mbili dhidi ya Angola inayokutana nao leo Jumatatu.
Katika michuano mitatu ya mwisho ya AFCON iliyoshiriki, Bafana Bafana imekuwa ikipoteza mechi zao za kwanza na haijapata ushindi wowote wa mechi ya ufunguzi kwa kipindi cha miaka 21 sasa, kitu kinachompa kazi kocha Hugo Broos mtihani mbele ya Palancas Negras.
Bafana Bafana na Angola zinakutana mjini Marrakech, huku Waangola wakiwa na kikosi chenye wachezaji kadhaa wenye uzoefu mkubwa katika michuano hiyo.
Bafana inaonekana kama ina nafasi nzuri zaidi ya ushindi, hasa kwa kuwa ni moja ya timu zilizofuzu Kombe la Dunia la 2026 na ilimaliza nafasi ya tatu katika AFCON iliyopita kule Ivory Coast, lakini kuna hatari kubwa ndani ya kikosi cha Angola ambacho hakiwezi kubezwa na Wasauzi.
Hapa chini ni wchezaji watano ambao Bafana Bafana wana kazi kubwa ya kuwachunga kama kweli inataka kutokana na ushindi na kuondoa gundu la kupasuka katika mechi za kwanza za AFCON.
Kialonda Gaspar
Huyu ni beki wa kati anayekipiga klabu ya Lecce ya Serie A ya Italia na amekuwa mchezaji wa kudumu katika kikosi cha Angola tangu alipoanza kuitumikia mwaka 2021.
Ni mchezaji mwenye nguvu, anayesoma mchezo vizuri, na huenda akapewa jukumu la kumdhibiti mshambuliaji pekee wa Bafana, iwe ni Lyle Foster au Evidence Makgopa.
Amecheza kila dakika ya msimu wa Serie A hadi sasa kwa Lecce, hivyo yuko katika kiwango kizuri na ana utimamu wa hali ya juu. Awali aliwahi kucheza ligi kuu ya Ureno na klabu ya Estrela.
Maestro
Jina lake linaeleza kila kitu. Kiungo mkabaji mwenye umri wa miaka 22 alikuwa sehemu ya kikosi cha Angola kilichoshiriki Kombe la Dunia la FIFA la U-17 mwaka 2019.
Baadaye alihamia Ureno na kujiunga na Benfica, ingawa hakupata nafasi katika timu ya kwanza.
Mwaka 2024 alihamia Uturuki, akichezea Adana Demirspor kabla ya kujiunga na klabu yake ya sasa, Alanyaspor, msimu huu.
Ana uwezo mkubwa wa kukaa mbele ya safu ya ulinzi na kuilinda, na licha ya kutokuwa mrefu sana, ana nguvu nyingi na bidii kubwa uwanjani.
Randy Nteka
Kiungo mshambuliaji aliyezaliwa Ufaransa ni mgeni wa hivi karibuni katika timu ya taifa ya Angola, akiwa amecheza mechi yake ya kwanza mwaka jana.
Ameitumikia klabu ya Rayo Vallecano ya LaLiga kwa misimu minne iliyopita, pamoja na kipindi cha mkopo Elche. Analeta ujanja, akili ya soka, na uwezo mzuri wa kufunga mabao.
Ingawa amepata muda mchache wa kucheza klabuni msimu huu, anajua AFCON ni jukwaa bora la kujithibitisha.
Pia alikuwa sehemu ya kikosi cha Angola kilichotwaa Kombe la COSAFA 2025 huko Bloemfontein.
Gelson Dala
Huyu ndiye tishio kubwa zaidi la mabao kwa Angola. Ni straika mzoefu aliyewahi kucheza kwa misimu kadhaa Ligi Kuu ya Ureno akiwa na Sporting Lisbon, ambako hakupata nafasi nyingi kabla ya kwenda Rio Ave kisha kuhamia Al-Wakrah ya Qatar.
Katika maisha yake ya klabu, amekuwa akifunga wastani wa bao moja kila mechi mbili. Ana historia nzuri dhidi ya Afrika Kusini, akiwa amewafunga mabao mawili hapo awali katika mechi za kufuzu CHAN na Kombe la Dunia 2015.
Katika AFCON iliyopita Ivory Coast, alifunga mabao manne, yakiwemo mawili dhidi ya Mauritania mengine dhidi ya Namibia.
Mabululu
Ni mshambuliaji mwenye mbinu za hila, ambaye licha ya kutokuwa mfungaji wa mabao mengi ana uwezo wa kuwasumbua mabeki na kutengeneza nafasi kwa wenzake, kwa mfano sawa na Makgopa kwa Bafana.
Amecheza kwa muda mrefu klabu kubwa za Angola kabla ya kujiunga na Al Ittihad ya Misri 2021, kisha kuhamia Al Ahli Tripoli ya Libya 2024.
Amekuwa akiingia na kutoka kwenye kikosi cha taifa tangu aanze kukitumikia mwaka 2013, lakini amecheza chini ya mechi 40 kwa kipindi cha miaka 12.
Alifunga mabao matatu katika AFCON iliyopita, likiwemo bao dhidi ya Namibia ambalo lililochaguliwa kuwa Bao Bora la Mwaka la CAF kutokana na ufundi wa hali ya juu aliouonesha.