Baba'ke Ndidi afariki ajalini
Muktasari:
- Klabu ya Besiktas, ambako Ndidi anachezea kwa sasa, ilithibitisha taarifa hiyo ya kusikitisha.
LAGOS, NIGERIA: BABA wa kiungo wa Nigeria, Wilfred Ndidi amefariki dunia katika ajali ya gari.
Klabu ya Besiktas, ambako Ndidi anachezea kwa sasa, ilithibitisha taarifa hiyo ya kusikitisha.
Klabu hiyo imeandika Jumanne asubuhi: “Tumepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kufariki dunia kwa baba mpendwa wa mchezaji wetu Wilfred Ndidi, Sunday Ndidi, aliyefariki katika ajali mbaya ya barabarani. Tunamuomba Allah amrehemu marehemu, na tunatoa rambirambi zetu za dhati kwa mchezaji wetu Wilfred Ndidi, familia yake na wapendwa wake.”
Ndidi mwenye umri wa miaka 29 alijiunga na klabu hiyo ya Uturuki majira ya joto yaliyopita kwa ada ya zaidi ya Pauni 10 milioni baada ya kuitumikia Leicester City kwa miaka minane.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Nigeria aliichezea Leicester City zaidi ya mechi 300, zikiwemo 220 katika Ligi Kuu England. Kwa muda mrefu alikuwa akihusishwa na uhamisho wa pesa nyingi kwenda Manchester United na klabu nyingine kubwa nchini England.
Mapema mwezi huu tu, Ndidi alikuwa akiichezea timu ya taifa ya Nigeria katika Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 huko Morocco.
Ndidi alicheza mechi nne kabla ya kupata jeraha lililomfanya akose nusu fainali dhidi ya Morocco, ambao baadaye walimaliza mashindano wakiwa washindi wa tatu. Hakushiriki mechi ya kuwania nafasi ya tatu dhidi ya Misri, lakini tayari ana jumla ya mechi 75 za kimataifa.
Ndidi alifunga bao katika ushindi wa 3-2 dhidi ya Tunisia kwenye hatua ya makundi huko Morocco na kulitoa bao hilo kwa baba yake, ambaye wakati huo alikuwa bado hai.
Kiungo huyo amesema: “Hili lilikuwa kwa ajili ya Papilo, gwiji Kanu Nwankwo. Nikiwa mdogo, baba yangu alikuwa shabiki mkubwa sana wa Kanu. Nyumbani kwetu, Kanu alikuwa shujaa wa kweli. Baba yangu alikuwa akizungumza kila mara kuhusu ustadi wake, mabao yake, na namna alivyoitumikia Nigeria.
“Kwa kweli nilijiambia kabla ya mechi kuwa nikifunga, nilipaswa kufanya hivyo kwa ajili ya baba yangu. Yeye ndiye aliyenisukuma kuingia kwenye soka na kunisimulia hadithi za wachezaji wakubwa. Kusherehekea kama Kanu nikiwa nimevaa jezi ya Super Eagles ni njia yangu ya kumshukuru baba yangu kwa msaada wake wote na kwa kunionyesha njia. Ni wakati wa kujivunia sana kwa familia yangu.”