AVB kuvaa buti za Redknapp Tottenham

LONDON, England ANDRE Villas-Boas amerejea tena Ligi Kuu England na sasa atafundisha timu ya Tottenham. AVB amepata kibarua hicho baada ya miezi minne ya bila kazi kufuatia kutemwa na Chelsea. Alikuwa akitazamiwa kwenda jijini London usiku wa Jumanne wiki hii kukamilisha mpango wake wa kufundisha dimba la White Hart Lane. Wiki ijayo atatambulishwa rasmi kwa vyombo vya habari kama kocha wa Spurs. Villas-Boas (34), anachukua nafasi ya kocha aliyetumuliwa Harry Redknapp. Redknapp alitimuliwa kazi baada ya kushindwa kuelewana na mwenyekiti wa klabu hiyo,Daniel Levy. Villas-Boas, anatarajia kusaini mkataba wa miaka mitatu, na atakuja sambamba na wasaidizi Jose Mario Rocha na Daniel Sousa. Katika makubaliano, atapewa pesa za kununua wachezaji wapya, huku jicho lake la kwanza likiwa kwa mchezaji Gylfi Sigurdsson anayetazamiwa kuitosa Liverpool na kujiunga na Spurs. Mlinzi wa Ajax, Jan Vertonghen ni chaguo la muda mrefu la Spurs, huku pia Villas-Boas akionyesha nia ya kutaka kumsajili mshambuliaji wa Chelsea, Daniel Sturridge na mlinzi wa Brazil, Oscar. Kazi yake kubwa ya kwanza itakuwa kumshawishiLuka Modric kubaki Spurs. Nyota huyo wa Croatia moyo wake umeegemea Real Madrid. Habari za ndani Spurs zinadai kuwa, klabu hiyo itafanya mazungumzo ya kumpata mshambuliaji Gonzalo Higuain iwapo watakubali kumruhusu Modric kwenda Bernabeu. Villas-Boas alifanya jitihada kubwa ya kutaka kumsajili mshambuliaji Higuain kutoka Argentina wakati akiwa kocha wa Chelsea. Bado kuna mashaka kama Higuain atakubali kuondoka Madrid na kujiunga na klabu ambayo haichezi mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.