Auba wa Gabon mambo mabaya
Muktasari:
- Waziri wa Michezo, Simplice-Desire Mamboula alitangaza hatua hizo baada ya kipigo cha mabao 3–2 kutoka kwa Ivory Coast, Desemba 31.
MARRAKECH, MOROCCO: SERIKALI ya Gabon imeivunja timu ya taifa, ikimpiga marufuku mshambuliaji Pierre-Emerick Aubameyang na kumfuta kazi kocha Thierry Mouyouma baada ya timu hiyo kutolewa kwenye Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025.
Waziri wa Michezo, Simplice-Desire Mamboula alitangaza hatua hizo baada ya kipigo cha mabao 3–2 kutoka kwa Ivory Coast, Desemba 31.
Gabon ilimaliza mkiani mwa kundi lao nchini Morocco baada ya kupoteza mechi zote tatu, ikianza na Cameroon, ikifuata Msumbiji na kisha Ivory Coast, kitu ambacho Mamboula amesema kuwa ni aibu.
Waziri huyo amesema: “Kwa kuzingatia kiwango cha aibu kilichoonyeshwa na Panthers kwenye Kombe la Mataifa ya Afrika, serikali imeamua kuvunja benchi la ufundi, kusimamisha timu ya taifa hadi hapo itakapotangazwa vinginevyo, na kuwatoa kwenye kikosi wachezaji Bruno Ecuele Manga na Pierre-Emerick Aubameyang.”
Gabon, ambao tayari walikuwa wameondolewa kwenye mashindano kabla ya mechi dhidi ya Ivory Coast, walipoteza uongozi wa mabao mawili mjini Marrakech.
Aliyekuwa mshambuliaji wa Arsenal, Chelsea na Barcelona, Aubameyang, hakushiriki mchezo wa mwisho wa kundi baada ya kurejea Marseille kwa ajili ya matibabu ya jeraha la paja.
Na Auba amesema: “Nadhani matatizo ya timu ni makubwa zaidi kuliko mimi kama mchezaji mmoja.”
Kocha Mouyouma alikuwa amehudumu kwa zaidi ya miaka miwili kidogo.
Zamani, ilikuwa kawaida kwa serikali za Afrika kuvunja au kusimamisha timu za taifa baada ya matokeo mabaya, lakini hali hiyo imekuwa nadra katika miaka ya hivi karibuni tangu FIFA ilipoanza kuchukua msimamo mkali dhidi ya kuingiliwa kwa serikali katika masuala ya soka.