Auba kutazama UEFA kwenye televisheni
LONDON, ENGLAND. PIERRE Emerick-Aubameyang amepigwa chini kikosi cha Chelsea cha Ligi ya Mabingwa Ulaya na kwa hasira ameamua kwenda zake Milan wakati timu ikiwa na mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Fulham usiku wa juzi Ijumaa.
Auba, 33, aliondoshwa kikosini ili kutoa nafasi kwa wachezaji wapya waliosajiliwa Januari. Chelsea ilinasa wachezaji wanane kwenye dirisha hilo na kanuni za Uefa kulikuwa na wachezaji watatu tu ndiyo waliokuwa wakiruhusiwa kwenye kikosi cha michuano hiyo.
Na katika hilo, Chelsea ilitaka wachezaji wake ghali Enzo Fernandez na Mykhailo Mudryk waingie sambamba na staa wa mkopo Joao Felix. Hivyo wachezaji David Datro Fofana, Noni Madueke, Andrey Santos, Gabriel Slonina na Benoit Badiashile wameshindwa kupata nafasi.
Kuondoka kwa Jorginho kumetoa nafasi moja, ambapo awali Chelsea ilikuwa imeorodhesha wachezaji 24 kati ya 25 wanaotakiwa. Hivyo, ili kuingiza watatu kwenye kikosi hicho cha Ulaya, kutokana na kuondoka Jorginho - Chelsea bado ilihitaji kumwondoa mchezaji mmoja na hapo ndipo jina la Auba lilipoondolewa ili Fernandez, Mudryk na Felix wapate nafasi.
Auba sasa atabaki kucheza kwenye Ligi Kuu England tu, huku hasira za kuondolewa zilimfanya aende zake Milan, ambako alipigwa picha akiwa na kaka yake juzi Ijumaa wakati chama lake lilikuwa na mechi dhidi ya Fulham iliyomalizika kwa sare ya bila kufunga.
Straika Auba alitua Stamford Bridge - Septemba mwaka jana na tangu wakati huo amefunga mabao matatu huku akianzishwa mara tisa tu chini ya kocha Graham Potter.
Kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, Chelsea itakipiga na Borussia Dortmund katika hatua ya 16 bora, Februari 15.