Arteta tabu iko pale pale
Muktasari:
- Kwa mujibu wa tovuti ya The Sun, kuelekea msimu ujao aina sawa sawa ya mpira unaochezewa sasa katika michuano ya Carabao msimu huu imeshatengenezwa na kupitishwa kwamba itachezewa katika EPL msimu ujao licha ya malalamiko yaliyopo sasa juu ya ubora wa aina hiyo ya mipira.
LONDON, ENGLAND: BAADA ya kuilaumu mipira inayotimika katika mechi zao za michuano ya Carabao kama sehemu ya wao kupoteza mchezo wao dhidi ya Newcastle, kocha wa Arsenal Mikel Arteta huenda akakumbana na balaa hilo hilo kwenye ligi kwa msimu ujao.
Kwa mujibu wa tovuti ya The Sun, kuelekea msimu ujao aina sawa sawa ya mpira unaochezewa sasa katika michuano ya Carabao msimu huu imeshatengenezwa na kupitishwa kwamba itachezewa katika EPL msimu ujao licha ya malalamiko yaliyopo sasa juu ya ubora wa aina hiyo ya mipira.
Arteta pia atakutana na aina nyingine ya mipira katika mchezo wao wa Jumapili ya wiki hii dhidi ya Manchester United katika mashindano ya Kombe la FA.
Mashindano hayo ya hutumia mipira kutoka kampuni ya Mitre na msimu huu itakuwa ni kwa mara ya kwanza wanachezea aina hiyo ya mipira mpya itakayoanza kutumika katika raundi hii ya tatu.
Kabla ya nusu fainali ya mkondo wa kwanza Jumanne dhidi ya Newcastle, kati ya mashuti 51 ya Arsenal kwenye Kombe la Carabao msimu huu, iliyopigwa kwa kutumia mipira hiyo iliyotengenezwa na Nike, 27 tu ndio ililenga lango (wastani wa asilimia 53).
Vilevile kwa upande wa Ligi Kuu kati ya mashuti 197 ya Arsenal, 102 yalikuwa yamelenga lango, wastani wa asilimia 52 kwa kutumia mpira wa Nike.
Na katika Ligi ya Mabingwa, Arsenal imepiga langoni mashuti 33 kati ya 57 ikiwa ni asilimia 58 kwa kutumia mipira ya Adidas.
Akijibu kauli ya Arteta juu ya udhaifu wa mipira inayotumika katika mashindano hayo, msemaji wa EFL, alisema: “Kama inavyohitajika katika mchezo wa kitaaluma, mpira wa PUMA unaotumika katika Kombe la Carabao msimu huu na mashindano ya EFL tangu 2021/22 ulijaribiwa kulingana na viwango vya FIFA na ukakidhi vigezo. Pamoja na Kombe la Carabao, mpira huo umefanikiwa kutumika katika ligi kuu za Ulaya, ikiwa ni pamoja na Serie A na LaLiga na ligi zetu tatu za EFL.”