Arteta na mkakati wa Gyokeres Arsenal
Muktasari:
- Arsenal imetumia Pauni 64 milioni kunasa huduma ya straika huyo ambaye alitoka kapa kwenye mechi ya kwanza ya Ligi Kuu England dhidi ya Manchester United, Jumapili iliyopita, ambapo hata shuti moja hakupiga kulenga goli.
LONDON, ENGLAND: KOCHA wa Arsenal, Mikel Arteta amewaambia wachezaji wake kwamba wanawajibika kuhakikisha straika Viktor Gyokeres anapata huduma bora ya kuonyesha makali yake.
Arsenal imetumia Pauni 64 milioni kunasa huduma ya straika huyo ambaye alitoka kapa kwenye mechi ya kwanza ya Ligi Kuu England dhidi ya Manchester United, Jumapili iliyopita, ambapo hata shuti moja hakupiga kulenga goli.
Na hilo limetokea baada ya Gyokeres kufanya mazoezi na wenzake kwa wiki mbili baada ya kujiunga na Arsenal akitokea Sporting Lisbon.
Straika huyo wa kimataifa wa Sweden alikuwa balaa kwa kufunga mabao huko Sporting, lakini bado ana kazi nzito ya kuzoea mazingira mapya kwenye Ligi Kuu England.
Lakini, Arteta hana wasiwasi juu ya uwezo wa straika wake huyo mpya na hivyo kuwataka wachezaji wenzake kuhakikisha wanamuwekea mazingira mazuri ya kuonyesha ubora wake.
Arteta alisema: “Nadhani tutakwenda kufurahi wote wakati atakapoanza kutumbukiza mipira kwenye nyavu kwa sbaabu huo ndio ubora.
“Hivyo, timu na mimi binafsi ni wajibu wetu sasa kumsaidia ili awe bora zaidi ndani ya uwanja na ile mechi ya kwanza ilikuwa na uhitaji mkubwa kwake."
Arteta alisema alifurahishwa na kiwango cha Gyokeres uwanjani Old Trafford kwa namna alivyokuwa akipambana na mabeki wa Manchester United.
Alimtoa uwanjani mapema kabla ya kufunga bao, na Arteta alisema alionekana kama kuna uwezekano wa mchezaji huyo kufunga.
“Nadhani mechi ile ilikuwa na uhitaji mkubwa sana wa kutumia nguvu na pia tulikuwa na Kai (Havertz) kwenye benchi. Nadhani sasa yupo vizuri.”
Mpango wa Arteta ulikuwa kumtumia Gyokeres na Havertz kwa pamoja, lakini staa huyo wa Kijerumani ameumia na hivyo atakuwa nje ya uwanja kwa siku kadhaa. Arsenal huenda ikakosa huduma ya Havertz kwa muda mrefu kutokana na maumivu yake ya goti kuona kama yatahitaji kufanyiwa upasuaji.
Arsenal ilikuwa na kasheshe zito la kuikabili Leeds United kwenye mchezo wa Ligi Kuu England uwanjani Emirates jana Jumamosi, ambapo macho ya wengi yalikuwa kwa straika Gyokeres kama atakuwa ameanza kutupia nyavuni.