Arteta katibua watu kisa ubingwa wa ligi

Muktasari:
- Kwa mara nyingine, Arsenal imetoka patupu ikielekea kumaliza nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu England kwa msimu wa tatu mfululizo, ikibwagwa na Manchester City kwenye misimu miwili iliyopita kabla ya kuwatokea tena hilo mbele ya Liverpool mwaka huu.
LONDON, ENGLAND: MASHABIKI wa Liverpool wamefyumu baada ya kocha wa Arsenal, Mikel Arteta kubeza ubingwa wao wa taji la Ligi Kuu England msimu huu. Kocha Arne Slot aliongoza Liverpool kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu England ikiwa ni msimu wake wa kwanza kuinoa timu hiyo ya Anfield.
Kwa mara nyingine, Arsenal imetoka patupu ikielekea kumaliza nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu England kwa msimu wa tatu mfululizo, ikibwagwa na Manchester City kwenye misimu miwili iliyopita kabla ya kuwatokea tena hilo mbele ya Liverpool mwaka huu.
Kuna uwezekano Arsenal ikashuka hadi kwenye nafasi ya tatu kama itashindwa kufanya vizuri katika mechi zake zilizobaki baada ya kuwa juu ya Man City kwa pointi tatu tu, hivyo Citizens wakishinda mechi zao wanaweza kumaliza katika nafasi ya pili.
Arsenal usiku wa Jumatano ilikuwa na majukumu kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, wakati ilipokwenda kurudiana na Paris Saint-Germain huko Parc des Princes katika mechi ya pili ya hatua ya nusu fainali.
Arteta alizinyooshea kidole pointi 82 ambazo zilitosha kuipa Liverpool ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu. Kikosi hicho cha Arteta kilimaliza nafasi ya pili kwenye msimu wa 2022/2023, kilipokusanya pointi 84 kabla ya kushika tena nafasi ya pili msimu uliofuata kwa kukusanya pointi 89. Kutokana na hilo, Arteta alisema Liverpool imepata bahati sana kushinda ubingwa wa msimu huu.
“Tulikuwa tunajaribu kushinda ubingwa msimu huu,” alisema Arteta.
“Kushinda mataji ina maana ya kuwa kwenye kipindi sahihi na wakati sahihi. Liverpool imebeba ubingwa ikiwa na pointi pungufu na zile tulizozikusanya sisi misimu miwili iliyopita. Kwa pointi zile zao, sisi kwa misimu miwili iliyopita tungekuwa na mataji mawili ya Ligi Kuu England.”
Hata hivyo, kauli hiyo imewatibua mashabiki wa Liverpool, ambao walianza kwa kumshambulia Arteta, ambapo shabiki wa kwanza alisema: “Niliona haya maneno na nadhani siyo yake.”
Mwingine alisema: “Natumai PSG itawabonda ili wamalize msimu mikono mitupu.” Na shabiki wa tatu alisema: “Huu ni ujinga mkubwa. Mwanzoni nilidhani ana akili.”
Shabiki wa nne aliongeza: “Liverpool imeshinda ubingwa ikiwa na bado na mechi nne; sasa bado mechi tatu, kuna uwezekano wa kuongeza pointi tisa, ambazo zitafikisha 91 kama watashinda zote. Arsenal ilikomea na pointi 89 na 84 katika mechi 38 ilizocheza kwenye misimu ya 23/24 na 22/23. Huyu jamaa akanywe tu chai.”
Shabiki wa tano alisema: “Arteta hajawahi kufikisha pointi 90. Liverpool ipo kwenye uwezekano wa kufikisha pointi 90 kwa mara ya nne katika kipindi cha miaka sita.” Mwingine alisema: “Arteta anaiaibisha klabu yake ambayo kuna wakati ilikuwa kubwa.”