Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Arteta: Hatujafanya vizuri msimu huu, tutasajili

ARTETA Pict

Muktasari:

  • Inaelezwa Arteta mwenyewe ndio hakutaka kusajili mastaa wengi katika dirisha lililopita jambo ambalo limemgharimu sana msimu huu, ambapo ameachwa mbali na mabingwa Liverpool na timu ikamaliza bila ya kushinda taji lolote.

LONDON, ENGLAND: KOCHA wa Arsenal, Mikel Arteta amefunguka kwamba timu yake itatumia fedha nyingi katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka huu, akikiri walifahamu kuwa kikosi chao hakikuwa bora vyakutosha msimu huu.

Inaelezwa Arteta mwenyewe ndio hakutaka kusajili mastaa wengi katika dirisha lililopita jambo ambalo limemgharimu sana msimu huu, ambapo ameachwa mbali na mabingwa Liverpool na timu ikamaliza bila ya kushinda taji lolote.

Mhispania huyu amesisitiza kwamba, anataka kusajili wachezaji wenye ubora wa hali ya juu kwenye kikosi chake kwa ajili ya msimu ujao, lakini pia anataka kusajili wachezaji wa ziada ili ikitokea suala la majeraha kuwe na uwezekano wa kuziba nafasi zilizoachwa na wale walioumia.

Arsenal wameweka nafasi ya mshambuliaji wa kati kuwa kipaumbele namba moja, na Arteta ni shabiki mkubwa wa Alexander Isak wa Newcastle United, huku mkurugenzi mpya wa michezo, Andrea Berta, akimpigia debe Viktor Gyokeres wa Sporting Lisbon.

Washika mitutu hawa,  pia wamekuwa wakimfuatilia kwa muda mrefu mshambuliaji wa RB Leipzig, Benjamin Sesko, hivyo mmoja kati ya hawa watatu anaweza kusajiliwa ikiwa ni katika mpango wa kutatua tatizo lao la kutokuwa na mshambuliaji wa kati wa kuaminika.

Kwa sasa pia wanadaiwa kufikia makubaliano ya kutoa Pauni 51 milioni kwa ajili ya kumsajili kiungo wa Real Sociedad, Martin Zubimendi, huku pia wakihitaji huduma ya winga wa kushoto wa Athletic Bilbao, Nico Williams.

Hata hivyo licha ya kupanga kuvamia soko na kusomba mastaa wenye uwezo mkubwa, Arteta pia amesisitiza kuwa watashikilia utamaduni wao na hawatatumia fedha kiholela bali watafanya  usajili sahihi. “Tutafanya kila tuwezalo kuboresha timu, tukianza na kuwaimarisha wachezaji tulionao kwenye timu, pia kusajili mchezaji yeyote sokoni ambaye tutaona atatupa ubora wa kutufanya kuwa washindi, hakika tutajaribu kufanya hivyo.”

Arteta pia amekiri kuwa msimu huu wameanguka sana na kurudi hatua moja kwenye Ligi Kuu England baada ya kushindwa kuendeleza ushindani dhidi ya Liverpool.

Moja ya sababu ambazo zimeonekana kuirudisha zaidi nyuma Arsenal kwa msimu huu ni mastaa wake kukumbwa na majeraha ya mara kwa mara ambayo yalisababisha wawe nje ya uwanja kwa muda mrefu.

Katika mechi kadhaa za Ligi Kuu, benchi lao lilionekana kuwa na idadi kubwa ya wachezaji wa kikosi cha pili ambao waliwekwa hapo baada ya wale wa kikosi cha kwanza kuumia.

Katika misimu miwili iliyopita, walikumbwa na majeraha machache zaidi, lakini msimu huu ni wachezaji wawili tu wa kikosi cha kwanza Declan Rice na William Saliba ndio walioweza kuanza mechi zaidi ya 30 katika Ligi Kuu England lakini waliobakia wengi walikosekana kwenye baadhi ya mechi kutokana na majeraha. Wachezaji 10 wa Liverpool wamecheza mechi zaidi ya 30 katika Ligi Kuu,  jambo lililowapa faida zaidi tofauti na wapinzani wao Arsenal.

“Tulijua tangu mwanzo kuwa kikosi chetu ni kidogo sana.”


“Tulikuwa na baadhi ya wachezaji waliokuwa na uwezekano mkubwa wa kuumia kutokana na rekodi yao ya majeraha kwenye misimu kadhaa iliyopita,” alisema Arteta.

“Tulijua hilo na hatukuweza kufanya chochote ili kubadilisha, lakini kawaida ili ushinde mataji lazima uwe na wachezaji ambao hawapati majeraha sana kwa msimu husika, Liverpool walikuwa na faida hiyo.”

Arteta pia alikiri kuwa alihisi wivu baada ya kuona sherehe za maadhimisho ya ubingwa wa Liverpool kwa sababu taji la mwisho la Arsenal lilikuwa Kombe la FA mwaka 2020.