Arteta apata ugumu warithi wa Partey, Jorginho

MAMBO yanaonekana kuwa magumu kwa Arsenal ambayo inapambana kusajili kiungo kuelekea dirisha lijalo ambapo wachezaji wote iliowaweka kwenye rada zao kuna ugumu kwenye kuwapata.

Hata hivyo, kwa sasa akili ya kocha wa timu hiyo, Mikel Arteta ni kupambana ili kushinda mechi zote zilizobakia na kuiombea mabaya Manchester City iangushe pointi na wao wachukue ubingwa.

Lakini jambo la pili ni kuboresha eneo lao la kiungo ambalo wachezaji wao wawili Thomas Partey na Jorginho wote wanaweza kuondoka mwisho wa msimu huu na mbadala wao ndio inaonekana kuwa changamoto.

Mchezaji wa kwanza ambaye ilimuweka katika rada zake ni kiungo wa Real Sociedad, Martin Zubimendi ambaye Arteta anamhusudu sana lakini mwenyewe amekanusha kunukia Arsenal.

Katika moja ya mahojiano, Zubimendi alisema hakuna mazungumzo yoyote aliyowahi kufanya na Arsenal na kinachoendelea ni tetesi tu ila yeye bado anajisikia furaha kuendelea kuichezea Sociedad.

Mbali ya maneno hiyo pia ugumu wa kumpata staa huyu unachagizwa na uwepo wa timu nyingi kubwa kama Bayern Munich na Barcelona ambazo pia zimeonyesha nia ya kutaka kumsajili.

Kwa mujibu wa tovuti ya Evening Standard, majina mengine yaliyo kwenye orodha ya Arteta  Bruno Guimaraes kutoka Newcastle United na kiungo wa Aston Villa, Douglas Luiz ambaye ilijaribu kuwasilisha ofa ya kutaka kumsajili katika dirisha lililopita lakini ilikataliwa.

Kwa upande wa Newcastle wanakumbana na ugumu kwa sababu timu hiyo haitaki kumuuza Guimaraes kama ilivyokuwa kwa Luiz.

Ingawa taarifa zilizoibuka siku za hivi karibuni zilifichua kwamba mabosi wa Newcastle wapo tayari kumuachia Bruno kutokana na uchumi wao lakini ada yake ya uhamisho haitopungua Pauni 100 milioni ambayo pia inaonekana kuwa changamoto kwa Arsenal kwa sababu inataka kupunguza matumizi ili kuepuka rungu kutoka mamlaka za soka kwa kukiuka sheria za matumizi ya pesa kwani imefanya usajili wa pesa nyingi katika kipindi cha hivi karibuni.

Hivyo mchakato wa kumpata kiungo mpya unaonekana kuwa mgumu kwao ingawa huenda wakawa na jina jingine baada ya msimu kumalizika.