Arteta alia kikosi chembamba

Muktasari:
- Hata hivyo, huo ulikuwa uamuzi wa Arteta mwenyewe kuwa na kikosi chembamba kwa sababu alihitaji mshikamano na umoja kwenye vyumba vya kubadilishia.
LONDON, ENGLAND: KOCHA wa Arsenal Mikel Arteta ameahidi kwamba dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi kikosi chake kitafanya usajili mkubwa kwa sababu msimu huu kilikuwa na kikosi chembamba.
Hata hivyo, huo ulikuwa uamuzi wa Arteta mwenyewe kuwa na kikosi chembamba kwa sababu alihitaji mshikamano na umoja kwenye vyumba vya kubadilishia.
Lakini, jambo hilo limemtokea puani kwa sababu Arsenal imekumbwa na majeruhi katikati ya vita ya kufukuzia ubingwa na hivyo kupigwa na Liverpool kwenye mbio za kubeba taji la Ligi Kuu England.
Na sasa kocha huyo wa Arsenal anataka kuongeza wachezaji wenye viwango kwenye kikosi chake cha Emirates kwa ajili ya msimu ujao, lakini akiweka wazi wanahitaji kuboresha namba zao za uwanjani.
Arsenal imeweka ubaoni orodha ya mastraika kadhaa kwenye mpango wao wa usajili, akiwamo mkali wa Newcastle United, Alexander Isak, ambaye ni kipenzi cha kocha Arsenal.
Lakini, bosi wa usajili, Andrea Berta, ambaye ni Mkurugenzi wa michezo, amekuwa kwenye mchakato wa kunasa huduma ya straika wa Sporting Lisbon, Viktor Gyokeres. Washika Bunduki hao wa London kwa muda mrefu pia wamekuwa wakimfukuzia sttraika wa RB Leipzig, Benjamin Sesko - hivyo mmoja kati ya washambuliaji hao wa kati watatua huko Emirates kwa ajili ya msimu ujao.
Arsenal inakaribia pia kunasa saini ya kiungo mkabaji wa Real Sociedad, Martin Zubimendi, wakati huo ikiwa kwenye msako pia wa winga wa kushoto na mkali wa Athletic Bilbao, Nico Williams.
Arteta alisema: “Tutafanya kila tunachokiweza kuboresha na kupandisha kiwango cha wachezaji walipo kwenye timu ili kuwa na uhakika wa kushinda kitu.”