Arteta afunguka kipigo cha Spurs
Muktasari:
- Arsenal ilikumbana na kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Spurs katika mchezo wao wa mwisho wa kirafiki wa pre-season uliofanyika huko Asia.
LONDON, ENGLAND: KOCHA, Mikel Arteta amesema kichapo ilichokipata kutoka kwa mahasimu wao Tottenham Hotspur kwenye mechi ya kirafiki huko Hong Kong kinawaamsha kwamba wanapaswa kuongeza nguvu kwenye maandalizi yao ya msimu mpya wa Ligi Kuu England kabla ya kuanza.
Arsenal ilikumbana na kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Spurs katika mchezo wao wa mwisho wa kirafiki wa pre-season uliofanyika huko Asia.
Arteta alisema: “Nina mtazamo chanya kwa kile kitu nilichokishuhudia kwa muda wa siku 10 zilizopita. Nimehamasika sana.
“Tupo mbele ya matarajio yetu kwenye maeneo mengi. Licha kwamba matokeo haya yametuacha kwenye hali mbaya, nadhani hilo litatuacha kwenye mtazamo chanya. Hapa tumeona mstari mwembamba uliopo baina ya kushinda na kushindwa, tuendelee kupambana.”
Arsenal ilitarajia kurejea London, jana Ijumaa kuendelea na mechi za pre-season kwenye uwanja wake wa nyumbani itakapokipiga na Villarreal na Athletic Bilbao kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu England, ambapo mechi ya kwanza itapigwa baina yao na Manchester United, Agosti 17.
Mechi ya Hong Kong dhidi ya Spurs, Arsenal ilimtumia straika wao mpya, Viktor Gyokeres kwenye mechi ya kwanza, alipoingia uwanjani akitokea benchini dakika 15 za mwisho. Na kocha Arteta anaamini straika huyo ataonyesha viwango bora.
“Ulikuwa muda mfupi, lakini walau amecheza mechi yake ya kwanza,” alisema Arteta na kuongeza:
“Muda mwingine, dhidi ya Villarreal uwanjani Emirates, nina hakika mambo yatakuwa tofauti.”
Kocha, Arteta alisifu pia kiwango cha beki wake mpya, Mreno Cristhian Mosquera, 20, kwa kuonyesha kiwango bora kwenye mechi ya Spurs.