Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Arteta afunguka hali ya Saliba

ARTETA Pict

Muktasari:

  • Saliba aliumia wakati wa mazoezi ya kupasha misuli ya kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu ya England dhidi ya Liverpool, kabla ya mapumziko ya ligi kupisha mechi za timu za taifa.

LONDON, ENGLAND: KOCHA wa Arsenal, Mikel Arteta ametoa taarifa za hivi karibuni kuhusu maendeleo ya beki wao kisiki, William Saliba, baada ya kutomjumuisha katika kikosi cha Arsenal kilichokabiliana na Nottingham Forest Jumamosi ya wiki iliyopita.

Saliba aliumia wakati wa mazoezi ya kupasha misuli ya kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu ya England dhidi ya Liverpool, kabla ya mapumziko ya ligi kupisha mechi za timu za taifa.

Majeraha hayo yalisababisha Saliba asijumuishwe katika kikosi cha timu ya taifa ya Ufaransa na ikaelezwa kwamba atakaa nje ya uwanja kwa wiki kadhaa.

Hata hivyo, Arteta alithibitisha kwenye mkutano wake na wanahabari Ijumaa kwamba Saliba alifanya mazoezi na kikosi siku hiyo asubuhi, jambo lililoongeza matumaini ya kwamba huenda angeanzishwa katika mchezo wa saa 6:30 mchana (kwa saa za England) dhidi ya Forest juzi Jumamosi.

Lakini kocha huyo wa Gunners alichagua kuwa mwangalifu zaidi na kumwacha nje, huku Cristhian Mosquera akipewa nafasi ya kuanza.

Aliiambia TNT Sports: "Alifanya mazoezi jana, lakini mwishoni mwa kipindi cha mazoezi hakuwa tayari kabisa kuanza mchezo."

Saliba alipata majeraha hayo wakati wa kupasha misuli kabla ya kipigo cha 1-0 dhidi ya Liverpool wiki mbili zilizopita. Ingawa alianza mchezo huo wa Liverpool, alilazimika kutolewa mapema.

Mosquera, ambaye alisajiliwa kutoka Valencia katika dirisha lililopita, aliingizwa akitokea benchini kumrithi Saliba kwenye Uwanja wa Anfield na alicheza vizuri.

Kisha alianzishwa dhidi ya Forest na kufunika kwa takwimu bora kabisa, mbele ya Piero Hincapie aliyesajiliwa na Arsenal katika siku ya mwisho ya dirisha la usajili akitokea Bayer Leverkusen.

Mchezo huo dhidi ya Nottingham ya Ange Postecoglou kwenye Uwanja wa Emirates ulikuwa wa kwanza baada ya mapumziko ya wiki mbili kwa ajili ya mechi za kimataifa.