Arteta achimba mkwara Arsenal, afungua milango kwa wachezaji wake
Muktasari:
- Arsenal leo ina mechi dhidi ya majirani zao Tottenham Hotspurs ugenini baada ya kushinda mechi mbili tu kati ya saba zilizopita katika Ligi Kuu England.
LONDON, ENGLAND: KOCHA wa Arsenal, Mikel Arteta amewaambia wachezaji wake kwamba mlango upo wazi na wanaweza kuondoka ikiwa hawawezi kuvumilia presha ya mbio za ubingwa.
Arsenal leo ina mechi dhidi ya majirani zao Tottenham Hotspurs ugenini baada ya kushinda mechi mbili tu kati ya saba zilizopita katika Ligi Kuu England.
Hiyo inajumuisha sare ya mabao 2-2 iliyopata dhidi ya Wolves, yenye hali mbaya katika msimamo Jumatano iliyopita.
Akijibu kuhusu jinsi anavyowasaidia wachezaji wake kupambana na presha kubwa wanayoipokea sasa, Arteta, amesema:
"Huwa nawauliza, 'Je, unataka kuwa sehemu ya presha au la?' Ikiwa mchezaji hataki namruhusu akafanye jambo jingine. Kila mtu amekuwa akisema kwa miaka kumi au kumi na tano kwamba tunapaswa kuchukua ubingwa baada ya kukaa kwa muda mrefu, lakini sasa tuko pale, tupo karibu kuchukua, ukiniambia kwamba presha inakuchanganya ndio maana huchezi vizuri, binafsi siwezi kukuelewa."
"Kelele na presha ni sehemu ya mbio za ubingwa, inatakiwa tuzoee, kwa sasa tunapambana na vyote kuhakikisha tunafanikisha lengo letu."
Katika mechi hiyo dhidi ya Arsenal, Spurs ilikuwa inaongozwa na Igor Tudor kwa mara ya kwanza baada ya kocha Thomas Frank kufukuzwa kazi mwanzoni mwa mwezi huu.
Arsenal ambayo kabla ya mechi ya Spurs ilikuwa kileleni kwa tofauti ya pointi mbili dhidi ya Man City, imekuwa na bahati mbaya sana katika misimu ya hivi karibuni ambapo hupoteza pointi katika dakika za mwisho.
Man City ya Guardiola ina historia ya kukusanya pointi nyingi zaidi katika misimu minne iliyopita katika mechi 12 za mwisho tofauti na Arsenal ambayo inatafuta taji lao la kwanza tangu mwaka 2004.
Akizungumzia hali ya ushindani kati ya timu yake na Man City, Arteta amesema: "Tunahitaji kufanya tunachotakiwa kufanya ni lazima ushinde mechi inayofuata, na ukifanya hivyo utakuwa katika nafasi nzuri zaidi. Hilo ndilo jambo pekee tunaweza kulifanya kwa sasa.
Tunahitaji kuishi katika hali ya sasa. Tulichofanya zamani hadi kuchukua ubingwa kilikuwa ni kizuri, lakini lazima tuishi katika hali ya sasa ambapo tunaonekana kuwa na nafasi kubwa ya kufanya jambo katika ligi na mashindano mengine."