Rice afichua alichoambiwa kuhusu London Derby
Muktasari:
- Maneno ya Saka kwa Rice yalikuwa mafupi na makali, lakini karibu miaka mitatu baadaye kiungo huyo wa England hajayasahau na kwa sasa yana ukweli zaidi kuliko wakati wowote, wakati Arsenal itakapokwenda ugenini kukwaana na Tottenham Hotspur, kwenye mechi muhimu ya kufikia ubingwa wa Ligi Kuu England, Jumapili.
LONDON, ENGLAND: KIUNGO ghali wa Arsenal, Declan Rice hakuwa hata na muda mrefu tangu kusaini kujiunga na The Gunners wakati Bukayo Saka alipomvuta pembeni na kuzungumza naye kuhusu umuhimu wa dabi ya Kaskazini mwa London.
Maneno ya Saka kwa Rice yalikuwa mafupi na makali, lakini karibu miaka mitatu baadaye kiungo huyo wa England hajayasahau na kwa sasa yana ukweli zaidi kuliko wakati wowote, wakati Arsenal itakapokwenda ugenini kukwaana na Tottenham Hotspur, kwenye mechi muhimu ya kufikia ubingwa wa Ligi Kuu England, Jumapili.
Kiungo Rice, alisema: “Nakumbuka Saka aliniambia: ‘Huwezi kupoteza dabi hapa dhidi ya Spurs’.
“Kwa mashabiki, kwa kila mtu, kwa wachezaji, kwa benchi la ufundi huo ndio mchezo ambao huruhusiwi kupoteza.”
Kwa hakika Arsenal hawawezi kuruhusu kupoteza mchezo wa Jumapili hii kwa gharama yoyote ile kutokana na umuhimu wake kwenye harakati zao za kumaliza ukame wa kunyakua taji la Ligi Kuu England.
Kikosi hicho cha Mikel Arteta kimeyumba katika mbio za ubingwa baada ya sare ya kushtua dhidi ya Wolves, Jumatano iliyopita. Na Arsenal itashuka ugenini kucheza na Spurs ikiwa bado kinara wa ligi, lakini pointi zinaweza kuwa chache kwa kuzingatia matokeo ya Manchester City katika mchezo wao wa Jumamosi dhidi ya Newcastle United.
Kikosi cha Pep Guardiola, Man City kitakuwa na mchezo mkononi na hilo litazidisha presha kwa Arsenal, ambayo imeshinda mechi mbili tu kati ya saba za mwisho kwenye Ligi Kuu England, hivyo piga ua itahitaji ushindi dhidi ya Spurs.
Dabi ya Kaskazini mwa London ni mchezo ambao Rice ameupenda tangu ajiunge na Arsenal mwaka 2023 na anajua ushindi wa safari hii ni muhimu zaidi. Kiungo huyo, ambaye hajapoteza katika mechi zake nne dhidi ya Spurs tangu aliponaswa na Arsenal, alisema: “Ingekuwa kubwa mno. Nilikuwa nimefungiwa katika dabi ya mwisho ya Kaskazini mwa London. Nimecheza mmoja tu huko Tottenham na mingine yote imekuwa Emirates. Ni moto sana. Uzoefu wangu wa kwanza huko White Hart Lane ulikuwa mkubwa sana. Tulikuwa tunaongoza 3-0 na wakarudi hadi 3-2. Unaanza kujiuliza: ‘Hii itaishia wapi?’
“Lakini, umati wa mashabiki, nguvu ya uwanja, unaweza kuihisi tu. Ni tofauti siku ya Dabi ya Kaskazini mwa London. Tumecheza vizuri katika miaka ya hivi karibuni, kwa hivyo tunapaswa kuendelea. Lakini itakuwa mechi ngumu kwa sababu watataka kutufunga baada ya mara ya mwisho tulipokutana. Hawakuwa na kikosi chao kamili wakati huo. Nina uhakika watakuwa tayari kabisa, kwa hivyo nasi tutakuwa tayari.”
Rice yuko sahihi kutarajia mwitikio kutoka Spurs, ambao walichapwa 4-1 na Arsenal walipokutana kwenye Uwanja wa Emirates, Novemba mwaka jana. Wenyeji pia wana kocha mpya, huku Igor Tudor akichukua nafasi ya Thomas Frank hadi mwisho wa msimu.
Uteuzi wa Tudor umebadilisha hali ya hewa ndani ya Spurs na changamoto kubwa kwa Arsenal itakuwa kukabiliana na mazingira ya uwanja, huku kocha huyo mpya akiwapeleka wachezaji wake kupata mlo wa usiku pamoja na kupanga mkakati wa kuidhibiti Arsenal.
Ukiweka kando kipute hicho cha dabi ya Kaskazini mwa London, Spurs itakapokuwa nyumbani kuwakaribisha mahasimu wao Arsenal, Jumapili hii zitashuhudiwa mechi nyingine za kibabe kwenye Ligi Kuu England, Crystal Palace itakipiga na Wolves, Nottingham Forest na Liverpool huku Sunderland ikimaliza ubishi na Fulham.
Rekodi zinazonyesha Spurs na Arsenal, zimeshakutana mara 67 kwenye Ligi Kuu England na 24 zilitoka sare, huku Spurs ikishinda 15, mara 13 nyumbani na mbili tu ugenini, wakati Arsenal imeshinda 28, mara 20 nyumbani na nane ugenini. Mechi tano zilizopita baina yao, Arsenal imeshinda nne na sare moja. Je, safari hii itakuwaje hasa kwa kauli ya Rice kwamba aliambiwa na Saka mechi ya Spurs sio ya kupoteza?