Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Arsenal inavyojiweka katika rekodi mbaya EPL

OSIM 01

Muktasari:

  • Baada ya kuporomoka kwao dhidi ya Wolverhampton Wanderers, matumaini yao ya ubingwa yako hatarini.

LONDON, ENGLAND: NDO hivyo. Arsenal ndio vinara wabovu zaidi wa Ligi Kuu England kuwahi kutokea katika muongo mmoja uliopita.

Baada ya kuporomoka kwao dhidi ya Wolverhampton Wanderers, matumaini yao ya ubingwa yako hatarini.

Arsenal ilikuwa inatafuta kurejesha hatima ya taji mikononi mwao, Jumatano usiku, lakini kupoteza mwelekeo mwishoni mwa mchezo kumefanya mbio za ubingwa kuwa wazi tena.

Kwa saa moja ya kwanza, mambo yalikuwa yanaenda vizuri katika kikosi hicho cha Mikel Arteta kilipoongoza kwa mabao 2-0 dhidi ya timu iliyopo mkiani, kutokana na mabao ya Bukayo Saka na Piero Hincapie.

Hata hivyo, bao la kuvutia la Hugo Bueno lililofungwa baada ya dakika ya 60 liliwasha upya mchezo, kisha Arsenal ikaporomoka katika ubora wake wa uwanjani.

Katika mkanganyiko wa nadra wa safu ya ulinzi, David Raya alishindwa kuudaka mpira wa krosi, huku Gabriel Magalhaes akijaribu kuondoa hatari.

Mpira uliomponyoka uliangukia kwa mchezaji wa Wolves, Tom Edozie, aliyeingia kutokea benchini na kuleta madhara dakika ya 94.

Shuti lake lilizuiwa kwenye mstari wa goli na Riccardo Calafiori, ambaye alikuwa ameingia uwanjani dakika moja tu iliyopita, kabla ya mpira huo kugonga mwamba na kisha kumgonga beki huyo na kutinga nyavuni.

ARS 04

Sare ya 2-2 ilisababisha Arsenal kupoteza pointi mbili muhimu na kubaki kileleni kwa tofauti ya pointi tano.

Hali hiyo ina maana wapinzani wao katika mbio za ubingwa, Manchester City, ambayo ina mchezo mkononi na bado hawajawakaribisha Arsenal kwenye Uwanja wa Etihad, inaweza kuwa mabingwa wa England iwapo kikosi cha Pep Guardiola kitashinda mechi zote zilizobaki.

Hii si mara ya kwanza hali kama hii kutokea. Msimu wa 2022/23, baada ya michezo 27, Arsenal iliongoza kwa pointi tano kabla ya kupitwa na Man City na kwenda kunyakua ubingwa huo.

ARS 02

Kwa kulinganisha kihistoria, timu hii ya Arsenal ambayo bado ipo katika mbio za kutafuta mataji manne, ina rekodi mbaya. Kwa kuzingatia pointi walizokusanya baada ya michezo 27, wao ndio vinara wabovu zaidi wa ligi katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.

Msimu wa 2015/16, Leicester City ilikuwa vinara pekee katika miaka 15 iliyopita waliokuwa na chini ya pointi 60 (56) baada ya michezo 27, kabla ya kwenda kutwaa ubingwa wao wa kihistoria.

Kwa upande mwingine, kiwango cha juu zaidi katika kipindi hicho kilifikiwa na Liverpool msimu wa 2019/20 chini ya Jurgen Klopp, ilipokusanya pointi 79 kati ya 81 zilizowezekana baada ya mechi 27.

ARS 03

Swali kubwa kwa mashabiki wa Arsenal; ni timu ngapi zilizoongoza baada ya mechi 27 na hatimaye kushinda taji?

Tangu msimu wa 2011/12, ni timu nne tu zilizoshindwa kutwaa ubingwa licha ya kuongoza msimamo wa ligi baada ya mechi 27, ambazo ni Chelsea (2013/14), Liverpool (2018/19), Arsenal (2022/23) na Liverpool (2023/24), huku tatu za mwisho zikipitwa na Man City.

Je, Arsenal watajiunga na orodha hiyo ya waliopoteza ubingwa licha ya kuongoza ligi hadi kwenye mechi ya 27?

ARS 01

Muda ndicho kitu kitakachoamua kama itafanikiwa kumaliza ukame wao wa takriban miaka 20 bila ubingwa wa Ligi Kuu England.

Kilicho wazi ni hawawezi kumudu makosa mengi zaidi kama watahitaji kubeba taji hilo na sasa kama Man City itashinda kiporo chake, itafanya pengo la pointi kubaki kuwa mbili pekee na bado miamba hiyo miwili haijakutana yenyewe uwanjani Etihad. Kazi ipo.