Arsenal yapigwa faini kisa gemu ya Man United
Muktasari:
- Sakata hilo limetokana na mgawanyo wa tiketi za timu ya ugenini, ambayo ni Man United.
LONDON, ENGLAND: ARSENAL imekumbana na adhabu ya kupigwa faini ya Pauni 500,000 baada ya kuvunja kanuni ya Kombe la FA katika mechi yao dhidi ya Manchester United, Januari mwaka huu.
Sakata hilo limetokana na mgawanyo wa tiketi za timu ya ugenini, ambayo ni Man United.
Man United ilipewa tiketi 8,000 kama timu ya ugenini kwenye mechi hiyo iliyofanyika uwanjani Emirates, ikiwa ni idadi ndogo tofauti na ilivyostahili kupewa.
Kanuni ya FA inafichua timu ya ugenini inapaswa kupewa walau asilimia 15 ya tiketi kwa kulinganisha na uwezo wa uwanja, ikiwa ni asilimia kubwa ya tiketi zinazotolewa kwenye mechi za Ligi Kuu England.
Man United ilipeleka malalamiko FA haikupewa tiketi 9,000 ilizopaswa kupewa, lakini Arsenal ilibainisha ilifanya hivyo kwa sababu za kiusalama.
Arsenal ilifichua jukwaa la juu uwanjani Emirates kwa upande wa timu za ugenini alitumiki kwa sababu za kiusalama. Lakini, FA ilipitia utetezi huo na kuchukua uamuzi wa kuipiga faini Arsenal kwa kuitoza Pauni 500,000.
Mchezo huo ulimalizika kwa Man United kushinda kwa mikwaju 5-3 ya penalti baada ya sare ya bao 1-1 katika muda wa kawaida na ule wa ziada. Kikosi hicho chini ya kocha Ruben Amorim ilisonga raundi ya nne na kuichapa Leicester City 2-1. Hata hivyo, Man United ilikwenda kukomea kwenye raundi ya tano baada ya kuchapwa na Fulham kwa penalti uwanjani Old Trafford. Arsenal na Man United zilikutana tena Machi na kutoka sare 1-1, Old Trafford.
Zimekutana tena kwenye mechi ya kwanza ya Ligi Kuu England msimu huu, ambapo Man United imekubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Arsenal, shukrani kwa bao la Riccardo Calafiori.
Ukiweka kando mechi ya Kombe la FA endapo kama zitapangwa kukutana, mechi nyingine ya Man United na Arsenal itapigwa Januari 24, mwakani.
Arsenal kwa sasa inaongoza msimamo wa Ligi Kuu England baada ya kukusanya pointi 16 katika mechi saba za kwanza.