Arsenal yapewa msala wa kupoteza muda Ligi Kuu England
Muktasari:
- Arsenal ilipata ushindi huo Jumatano kutokana na bao la mapema la Bukayo Saka, katika mechi yake ya 300 akiwa na klabu hiyo, lakini gumzo ni jinsi ilivyokuwa ikichelewesha kuanzisha mpira kwa maana ya kupoteza muda katika nyakati wa kurusha mpira, kupiga faulo au kona.
LONDON, ENGLAND: ARSENAL ilitumia zaidi ya dakika 30 kuanzisha mchezo upya katika ushindi wao wa 1-0 dhidi ya Brighton, ushindi uliowasaidia kusogea karibu zaidi na ubingwa wa Ligi Kuu England.
Arsenal ilipata ushindi huo Jumatano kutokana na bao la mapema la Bukayo Saka, katika mechi yake ya 300 akiwa na klabu hiyo, lakini gumzo ni jinsi ilivyokuwa ikichelewesha kuanzisha mpira kwa maana ya kupoteza muda katika nyakati wa kurusha mpira, kupiga faulo au kona.
Hata hivyo, baada ya kushindwa kufunga bao la pili, kikosi cha Mikel Arteta kililazimika kulinda ushindi huo mwembamba, jambo lililomkasirisha Kocha wa Brighton, Fabian Hurzeler pamoja na mashabiki wengi waliokuwepo katika Uwanja wa Amex.
Hurzeler, mwenye umri wa miaka 32, alimshambulia vikali Arteta na timu yake baada ya mchezo, aliposema: “Kulikuwa na timu moja tu iliyojaribu kucheza mpira wa miguu kwenye ile mechi. Nina swali moja: je, umewahi kuona mchezo wa Ligi Kuu kipa anaanguka chini mara tatu? Mimi sitakuwa kamwe kocha anayejitahidi kushinda kwa njia hiyo.
“Ligi Kuu inapaswa kuweka sheria zilizo wazi zaidi, iweke mipaka kuhusu kupoteza muda, kwa sababu wanapaswa pia kuwalinda waamuzi. Unaweza kuona wazi wanafanya kila kitu sasa ili kushinda mchezo huu na mwishowe yote yanahusu sheria. Kwa sasa nahisi kama wanatengeneza sheria zao wenyewe bila kujali wanachezaje. Ndiyo maana ni vigumu kuhukumu hali hiyo.
“Ni kweli kila timu wakati mwingine hupunguza kasi au kupoteza muda, lakini lazima kuwe na kikomo na kikomo hicho kinapaswa kuwekwa na Ligi Kuu. Waamuzi wanapaswa kuweka mipaka. Kwa sasa wanafanya wanachotaka. Kama Ligi Kuu na waamuzi wanaruhusu kila kitu, basi timu zitaunda sheria zao wenyewe. Sitaki kupoteza muda wangu kuzungumzia hilo.
“Ukiuliza kila mtu hapa kama alifurahia mchezo huu, labda mtu mmoja tu ataunyoosha mkono, labda shabiki mkubwa wa Arsenal. Kama wakishinda Ligi Kuu, hawatajali walivyoshinda na unaweza kuona wanafanya kila kitu kushinda ubingwa huo.”
Hasira za Hurzeler zinaonekana kuwa na msingi, kwani imebainika kuwa Arsenal ilitumia jumla ya dakika 30 na sekunde 51 kuanzisha mchezo upya katika Uwanja wa Amex. Muda uliopotezwa na Arsenal katika mechi hiyo ilikuwa kwenye kona tatu, faulo 14 na mipira ya kurusha 24.
Hii ni mara ya pili msimu huu kwa Arsenal kutumia zaidi ya nusu saa kuanzisha mchezo upya, baada ya tukio kama hilo kutokea katika ushindi wao wa 1-0 dhidi ya Fulham, Oktoba mwaka jana.
Kwa jumla, Arsenal imetumia saa mbili na dakika saba wakisubiri kupiga kona katika msimu huu wa Ligi Kuu England.
Lakini cha kushangaza ni Arsenal si timu inayopoteza muda zaidi katika ligi hiyo. Kwa kweli kuna timu tano zinazochukua muda mrefu zaidi kwa wastani kuanzisha mchezo baada ya mpira kutoka nje.
Kwa wastani; Arsenal hutumia sekunde 30.2 kila mpira unapokuwa nje ya mchezo. Lakini, Sunderland inaongoza kwa kutumia sekunde 33.1, Brentford sekunde 32.3, Crystal Palace sekunde 31.2, Newcastle United sekunde 30.8 na Leeds United sekunde 30.4
Chini kidogo ya Arsenal katika orodha hiyo ni Burnley, Aston Villa, Tottenham Hotspur, Chelsea na West Ham United.
Brighton iko karibu mwisho wa orodha wakitumia wastani wa sekunde 26.5 kuanzisha mchezo upya.
Wakati huo huo, Liverpool ndiyo timu inayopoteza muda kidogo zaidi kwenye Ligi Kuu England. Mabingwa hao watetezi hutumia wastani wa sekunde 25.8 kuanzisha mchezo kila mpira unapokuwa nje.
Licha ya kuwa wa nne katika orodha ya timu zinazopoteza muda, Newcastle ilivunja rekodi ya muda mwingi zaidi mpira ukiwa nje katika mechi moja ya Ligi Kuu England ilipocheza dhidi ya Liverpool, Agosti mwaka jana.
Katika mechi hiyo, Newcastle ilitumia zaidi ya dakika 37 wakipoteza muda katika Uwanja wa St James’ Park kabla ya kupoteza 3-2 baada ya bao la dakika za mwisho la Rio Ngumoha.
Arteta hatajali sana maneno ya wapinzani kuhusu mbinu za timu yake iwapo Arsenal itafanikiwa kushinda ubingwa, Mei mwaka huu. Arsenal imeweka nia ya kumaliza ukame wa miaka 22 bila ubingwa wa Ligi Kuu England. Pia bado iwapo kwenye mbio za kusaka ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Kombe la FA na Kombe la Ligi.
Ushindi wa Jumatano uliifanya Arsenal kuongeza pengo la pointi kileleni na kufikia saba baada ya Manchester City kutoka sare ya 2-2 dhidi ya Nottingham Forest. Alipoulizwa kuhusu malalamiko ya Hurzeler juu ya kupoteza muda kwa Arsenal, Arteta alijibu kwa kifupi: “Kipi kinashangaza hapo.”