Arsenal yaichapa Spurs, yakomaa kufukuzia ubingwa

LONDON, ENGLAND
ARSENAL imeichapa Tottenham Hotspur 3-2 na kuendelea kubaki kwenye kilele cha msimamo wa Ligi Kuu England baada ya kuonyesha kiwango bora kwenye North London derby.
Pierre Emile Hojbjerg alijifunga kuwapa bao la kuongoza Arsenal, kabla ya Bukayo Saka kuwafanya vijana hao wa Mikel Arteta kuongoza kwa mabao mawili.
 
Kai Havertz aliruka juu kufunga mpira wa kona na kuifanya Arsenal kuongoza mabao 3-0 kabla ya mapumziko na kuonekana kama mambo yangekuwa magumu zaidi kwa mahasimu wao hao wa London, Spurs.

Lakini, kipindi cha pili, Spurs ilipambana kutafuta namna ya kujinasua kwenye kipigo kizito. Christian Romero na Heung-min Son walifunga na kufanya ubao wa matokeo kusomeka 3-2, na ulibaki hivyo hadi filimbi ya mwisho.

Matokeo hayo yanaifanya Arsenal kufikisha pointi 80 na kuendelea kubaki kwenye kilele cha msimamo wa Ligi Kuu England huku wakiombea mabaya yaikute Manchester City kwenye mbio zao za ubingwa.

Man City, ambao ni mabingwa watetezi walikuwa na kibarua cha kuikabili Nottingham Forest. Ushindi wa vijana wa Pep Guardiola kwenye mchezo huo utawafanya wafikishe pointi 79, huku wakiwa na mchezo mmoja mkononi.

Vikosi vilianza hivi;
Tottenham
:  Vicario; Porro, Romero, Van de Ven, Davies; Hojbjerg, Bentancur; Kulusevski, Maddison, Werner; Son

Arsenal: Raya; White, Saliba, Gabriel, Tomiyasu; Partey, Rice, Odegaard; Saka, Havertz, Trossard.